Saturday, 18 August 2018

Waziri Azuia Umeme Kuruka Nyumba za Tembe
WAZIRI wa Nishati, Dk. Merdad Kalemani, amewataka wakandarasi wote nchini wanaotekeleza mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), kuhakikisha wanaweka umeme katika nyumba zote zikiwamo za tembe huku akipiga marufuku kurukwa.

Akizungumza wakati akiwasha umeme katika vijiji vya Lukungu, Nyakaboja na Bukabile vilivyoko Wilaya ya Busega, Simiyu, alisema wamekuwa wakipata taarifa za wakandarasi waliopewa kazi ya kutekeleza mradi huo kuwa wamekuwa wakiziruka nyumba hizo kwa madai hazifai kupata huduma hiyo.

Aliwataka wakandarasi hao kuhakikisha wanapeleka umeme katika kila kijiji na kila kitongoji ili wananchi waweze kuondokana na adha kubwa wanayokumbana nayo ya kukosa nishati ya umeme.

“Nimepata taarifa kuwa wananchi wenye nyumba za tembe wanarukwa, maagizo yangu ni marufuku kuruka nyumba ya tembe, tena nyumba hizo zipewe kipaumbele cha kwanza kupata umeme na hakuna kuruka kijiji, kitongoji au nyumba yoyote,” alisema Kalemani.

Alisema Serikali haitaongeza muda, siku wala saa kwa mkandarasi yeyote atakayeshindwa kutekeleza mradi huo kwa muda mwafaka waliopewa na Tanesco na aliwataka kutekeleza mradi huo hadi kukamilika kwake kwa muda mwafaka.

Alisema mkandarasi White City anayetekeleza mradi huo Simiyu kasi yake ni ndogo na alimtaka kuongeza kasi zaidi ili kuhakikisha vijiji 152 mkoani humo vinapata umeme.

Alisema katika Wilaya ya Busega kupitia mradi huo vijiji vyote 54 vilivyoko wilayani humo vitapata umeme na aliwataka wananchi kuhakikisha wanalipia gharama ya Sh 27,000 ili kupatiwa huduma hiyo.

Pia alizitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafunga mfumo wa umeme katika taasisi za umma zikiwemo shule na vituo vya kutolea huduma za afya.

“Wakati sisi tukihangaika kuleta umeme kwa kila mwananchi, niwatake wakurugenzi wa halmashauri pamoja na madiwani kupitia vikao vyao, watenge bajeti kuhakikisha taasisi zote za umma zinafungiwa mfumo mzima wa umeme kwa ndani,” alisema Kalemani.

Awali, Mbunge wa Busega, Dk. Rafel Chegeni, alisema bado kuna baadhi ya vitongoji na vijiji vimerukwa na mkandarasi anayetekeleza mradi huo.

Dk. Chegeni alisema kilio kikubwa cha wananchi wa jimbo hilo ni ukosefu wa umeme na alimwomba Kalemani kutatua changamoto hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.
Spika Ndugai: Hakuna Tatizo Wabunge na Madiwani Kuhama Vyama.....Ndo Kuimarika kwa Demokrasia
Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema ni ruhusa kwa viongozi wa vyama vya siasa kuhama chama kwani huko ndio kuimarika kwa demokrasia. 

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua semina kwa ajili ya kamati za uongozi, Wenyeviti na Makamu wenyeviti katika Ofi si ya Bunge Tunguu Wilaya ya kati Unguja alisema hakuna vikwazo wala pingamizi kwa viongozi wa vyama vya siasa ikiwemo wabunge kuhama vyama.

Alisema kinachofanyika kwa sasa katika matukio ya wabunge kuhama chama na kuhamia kwingine ni mchakato wa kuimarika na kupanuka kwa demokrasia nchini. 

“Ni ruhusa kwa mbunge yoyote kuhama chama chake na kujiunga na chama anachoona kinamanufaa kwake,” alisema. 

Alisema wimbi la viongozi wa vyama vya siasa kuhama vyama hakumaanishi kwamba kutaua demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini.

“Unajua kitendo wanachokifanya ni sawa na kutoka nje kunywa chai na baadaye kurejea ukumbini,” alisema. 

Awali, spika alizitaka taasisi mbili zilizopewa majukumu ya kutunga sheria kushirikiana kwa sababu kazi zao zinafanana. 

Alisema Baraza la Wawakilishi kazi yake kutunga sheria wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano linafanya kazi kama hizo za kuwawakilishi wananchi katika majimbo ya uchaguzi.

“Vyombo vyetu vya kutunga sheria vinatakiwa kushirikiana kikamilifu kwa sababu majukumu yake yanafanana ya kuwakilisha wananchi katika majimbo ya uchaguzi,” alisema. 

Aidha Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid alisema majukumu ya vyombo hivyo ni kuwatumikia wananchi. 

“Ushirikiano wa vyombo hivi ambavyo ni mhimili wa tatu wa dola ni muhimu ikiwa ni Wawakilishi wa wananchi katika majimbo ya uchaguzi,” alisema.
Katibu Mkuu CCM Dkt. Bashiru Ali Atoa Onyo Kwa Wanaosaka Urais Zanzibar
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. Bashiru Ali amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho, kufuta ndoto walizokuwa nazo za kutaka kushika madaraka ya urais wa Zanzibar licha ya kuwa muhusika yupo na muda wake haujakwisha kwa mujibu wa sheria.

Dkt. Dkt. Bashiru ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anazungumza kwenye mkutano wa hadhara wa CCM huko visiwani Zanzibar katika ziara yake ya kazi baada ya kusikia tetesi, kuwa kuna baadhi ya viongozi wa CCM wameanza kuunda makundi yenye lengo la kutaka kumtoa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein.

"Wapo watu nasikia wengine wana vyeo na wengine hawana, wana ndoto ya kushika madaraka ya urais wa Zanzibar hiyo nafasi haijatangazwa kuwa wazi bado ina mwenyewe. 

"CCM sio chama cha kusaka vyeo ni chama cha mapinduzi, wafuata vyeo 'wakome'. Tutaendelea kuwafuatilia wengine tunawajua na siku zenu zinahesabiwa. 

"Muacheni Rais Shein amalize kipindi chake kwa heshima. Wakazi ukifika tutasema na kuweka utaratibu", amesema Dkt. Bashiru.

Pamoja na hayo, Dkt. Bashiru ameendelea kwa kusema "kiongozi mzuri haundi makundi kutafuta cheo, bali anasubiri kuombwa na watu kwasababu wanaomuomba ndio wanaomjua.

 "Wewe hujijui na wapo wengine ukiangalia orodha hata ukimpa ukuu wa wilaya hauwezi halafu anataka kuutafauta urais".

Aidha, Dkt. Bashiru amebainisha kwamba endapo nafasi hiyo ya urais itakuwa wazi basi wataitangaza kwa mujibu wa sheria kufuatana na chama chao kinavyosema na sio kupitia makundi ya watu yanayoendelea mahotelini.

Dkt. Bashiru Ally Kakurwa tokea alipoteuliwa mnamo Mei 29, 2018, hii ndio ziara yake ya kwanza kufika visiwani Zanzibar na kutoa kauli kama hizo kwa watu wenye lengo la kutaka kushika nyadhfa za urais bila ya kufuata sheria isemavyo.
DK. SEMAKAFU AKEMEA VITENDO VYA UNYANYAPAA DHIDI YA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUMU

Naibu Katibu Mkuu Dk. Avemaria Semakafu amewataka walimu wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu Kuacha vitendo vya unyanyapaa kwa wanafunzi hao, kwa kuwa taaluma waliyonayo inahitaji upendo na uvumilivu.

Dk. Semakafu ametoa kauli hiyo mkoani Mwanza wakati akizungumza na walimu hao ambao wanashiriki mafunzo maalumu ya ya siku 10 ya kuchambua mtaala uliobireshwa yenye lengo la kuwajengea uwezo walimu wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wa akili, wasioona na wanafunzi viziwi.

Dk. Semakafu pamoja na mambo mengine amewataka walimu kuacha masuala vitengo na badala yake walimu wafanye Kazi zao kwa weledi, ikiwa ni pamoja na kuwa wanaharakati katika masuala ya Elimu.

“ Walimu naomba niwaambie ukweli huko kwenye shule zetu tumeanzisha vitengo ambavyo havina sababu yoyote na tumekuwa hatufanyi Kazi zetu kwa weledi, wengine hatufundishi kwa visingizo vya kuwa tunasimamia vitengo, tuache mara moja na badala yake tufundishe watoto wetu kwa weledi,”alisisitiza Dk. Semakafu.

Katika mafunzo hayo baadhi ya Walimu wakata kufahamu kuhusu suala la wanafunzi kuishia Darasa la Sita ambapo Dk. Semakafu alieleza kuwa Elimu inaongozwa na Sheria na Sheria yetu Elimu Msingi ni miaka Saba hivyo Sheria ya Elimu haijabadilika.

Mafunzo hayo yanashirikisha walimu 132 wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu kutoka mikoa wa Kagera, Geita , Kigoma,Mara,Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Rukwa na Tabora.

Imetolewa na:
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA  YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
18/8/2018

Friday, 17 August 2018

HOSPITALI YA WILAYA YA NYAMAGANA YAPOKEA SARUJI MIFUKO 50.

Mbunge Jimbo la Nyamagana Mhe Stanslaus Mabula hivi leo amekabidhi mifuko 50 ya Saruji katika Hospital ya wilaya ya Nyamagana Butimba msaada kutoka kwa mdau  wa maendeleo Mwanza Huduma. Mhe Mabula amesema Saruji hiyo inathamani shillingi 875,000 isaidie ujenzi wa uzio ili kuweka mazingira salama ya hospitali.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wilaya ya Nyamagana Dkt Kajiru Eliamani amemshukuru Mhe Mabula kwa jitihada zake za  uboreshaji miundombinu ya hospitali, amemhakikishia msaada kujenga uzio wa hospitali hiyo kama ilivyokusudiwa.

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Nyamagana🇹🇿
Chadema yaanika majina ya wagombea wake uchaguzi mdogo

Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), kimetangaza majina ya wagombea wake watakaowania ubunge katika majimbo ya Ukonga, Korogwe Vijijini na Monduli kupitia kikao cha kamati kuu ya chama.

Katibu wa chama hicho kanda ya kaskazini Amani Golugwa ameiambia tovuti ya www.eatv.tv kuwa tayari chama hicho kupitia mkutano wake kimekwisha pitisha majina ya watakaopeperusha bendera za chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Septemba 16, 2018.

Golugwa amewataja wagombea hao kuwa ni Amina Ally atakayegombea ubunge jimbo la Korogwe Vijijini, aliyekuwa Diwani wa kata ya Lepurko Yonas Masiaya Laizer atasimama jimbo la Monduli pamoja na Asia Msangi atakayeiwakilisha Chadema jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo matatu na wa udiwani katika kata mbili za Tanzania Bara utakaofanyika Septemba 16, mwaka huu.

“Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Ubunge katika majimbo matatu majimbo hayo kuwa ni Korogwe Vijijini, Mkoa wa Tanga kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Stephen Hilary Ngonyani, Jimbo la Ukonga katika mkoa wa Dar es Salaam na Jimbo la Monduli mkoani Arusha baada ya waliokuwa wabunge wa majimbo hayo kujiuzulu uanachama wa CHADEMA hivyo kukosa sifa za kusalia wabunge”, ilisema taarifa ya tume.

Uchaguzi huo utafanyika ikiwa ni mwezi mmoja kupita tangu ufanyike uchaguzi mwingine mdogo katika jimbo la Buyungu wilayani Kakonko mkoani Kigoma pamoja na kata 79 nchini ambapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kilishinda kwa asilimia 100%.
MISA TANZANIA,INTERNEWS ZAWANOA WAANDISHI WA HABARI GEITA,SIMIYU NA SHINYANGA
Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Tawi la Tanzania kwa kushirikiana na Internews Tanzania wameendesha mafunzo kwa waandishi wa Habari Kanda ya Kaskazini/Magharibi (Geita, Shinyanga na Simiyu) kuhusu Changamoto za Sheria mpya za habari.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoanza Agosti 17,2018 hadi Agosti 18,2018 yanafanyika katika ukumbi wa Alpha Hotel Mjini Geita.
Akifungua Mafunzo hayo,Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Tawi la Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa alisema kupitia mafunzo hayo waandishi wa habari watajengewa uelewa kiuhusu sheria mbalimbali zinazohusu vyombo vya habari na waandishi wa habari na namna waandishi wa habari wanavyoweza kuishi na sheria hizo.
"Lengo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari na kuangalia changamoto zinazotolewa na sheria hizi sambasamba na kukumbushana miiko ya uandishi wa habari lakini pia kufahamu nafasi ya mwandishi wa habari kama mtetezi wa haki za binadamu",alisema.

Naye Afisa Mradi wa Boresha Habari kupitia Shirika la Internews linalofadhiliwa na USAID Victoria Rowan aliwasihi waandishi wa habari waliopata fursa ya kushiriki mafunzo hayo kutumia vyema elimu wanayopewa. 

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Tawi la Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari mikoa ya Geita Shinyanga na Simiyu kuhusu Sheria za vyombo vya habari katika ukumbi wa Alpha Hotel Mjini Geita - Picha zote na Kadama Malunde & Joel Maduka
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Tawi la Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa akielezea malengo ya semina hiyo
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Tawi la Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa
Afisa Mradi wa Boresha Habari kupitia Shirika la Internews  Victoria Rowan akizungumza wakati wa mafunzo hayo
Afisa Mradi wa Boresha Habari kupitia Shirika la Internews  Victoria Rowan akielezea jambo ukumbini
Mwezeshaji katika Mafunzo hayo,Wakili James Marenga akitoa mada kuhusu Sheria ya  Huduma za Habari
Mwezeshaji katika Mafunzo hayo,Wakili James Marenga akifafanua vifungu mbalimbali vya sheria
Kushoto ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga,Kadama Malunde ambaye pia ni Mkurugenzi wa Malunde1 blog akifuatilia mada ukumbini.Kulia ni Bahati Sonda kutoka mkoani Simiyu
Mwandishi wa habari Salma Mrisho kutoka Geita akichangia mada
Mwandishi wa habari Paschal Michael kutoka mkoa wa Simiyu akichangia hoja ukumbini

Mwandishi wa habari Rehema Matowo kutoka Geita akichangia mada 
Semina inaendelea
Waandishi wa habari wakiwa ukumbini
Kushoto ni Mwandishi wa habari Rose Mweko kutoka mkoani Geita akiwa na Derick Milton kutoka Simiyu na Editha  Edward kutoka Geita
Washiriki wakifuatialia mada ukumbini
Semina inaendelea
Washiriki wakifuatilia mada 
Mafunzo yanaendelea
Mwandishi wa habari Joel Maduka (kulia) kutoka Geita na Bahati Sonda kutoka Simiyu wakiwa ukumbini
Mwandishi wa habari Stella Ibengwe kutoka Shinyanga akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo
Mwandishi wa Habari Rehema Evance kutoka Simiyu akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo
Mwandishi wa habari Osman Nyamiti kutoka Divine Fm Shinyanga akichangia mada ukumbini
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Geita, Daniel Limbe akizungumza wakati wa mafunzo hayo.

Kikwete amtembelea tena Kingwangalla, Sasa kuruhusiwa muda wowote

RAIS Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete amemtembelea na kumjulia hali Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla aliyelazwa katika wodi maalum kitengo cha Taasisi ya Mifupa MOI, hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa mara nyingine tena.

Hii inakuwa ni mara ya tatu kwa Kikwete kumtembelea Dk Kigwangalla ambapo awali alimtembelea Agosti 8, 2018 alipokuwa amelazwa Wodi ya Mwaisela akipatiwa Matibabu ya awali na juzi Agosti 15, 2018 katika wodi ya Taasisi ya Mifupa MOI.

Akiwa hospitaini hapo mapema jana, Kikwete ameweza kumjulia hali na kubadilishana nae mawazo mbalimbali huku akimtakia unafuu aendelee na majukumu yake ya kila siku na akimpongeza kwa shughuli zake anazozifanya katika kuinua sekta ya Utalii pamoja na kulinda rasilimali za Maliasili.

“Nikutakie kheri. Nashukuru kwa kukuta unaendelea vizuri sasa na nilikuja ukiwa upo unaongea ukiwa umelala kitandani na kwa sasa nimekuja tena umeweza kuimarika na hata kutembea na kukaa kama hivi hongera sana” alieleza Kikwete wakati akimjulia hali Waziri Kigwangalla wodini hapo.

Tayari jopo la Madaktari bingwa wa MOI wamebainisha kuwa Dkt. Kigwangalla kwa sasa anaendelea vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani ambapo kwa sasa sehemu zilizobakia ni mkono wake wa kushoto ambao kila siku unaendelea kuimarika.

Hata hivyo, Dkt. Kigwangalla amemweleza Kikwete kuwa kwa sasa hali yake inaendelea kuwa vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani huku akiendelea na mazoezi kidogokidogo.

Aidha, jioni ya jana Dkt. Kigwangalla ameweza kufanya mazoezi ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa moja kuanzia kwenye viunga vya Hospitali hiyo na kuzunguka maeneo yanayozunguka Muhimbili na baadae kupanda kwa kutumia ngazi katika jengo anapopatiwa matibabu kwa miguu mpaka gorofa ya sita.

Waziri Dkt. Kigwangalla alipata ajali ya gari mnamo Agosti 4, 2018 huko Manyara akiwa katika ziara ya kikazi ambapo katika ajali hiyo iliyokuwa na watu 6, Afisa Habari wa Wizara hiyo Hamza Temba alifariki dunia huku watano wakijeruhiwa akiwemo yeye anaendelea na matibabu Hospitalini hapo.