Mwandishi wetu,Arusha


Waziri wa nishati ,January Makamba ameagiza kuondolewa Mara moja afisa habari wa shirika la umeme nchini(Tanesco) huku akiagiza kuvunjwa kwa idara ya uhusiano wa shirika hilo na kuwekwa watu wapya.


Mbali na agizo hilo pia amegiza  hatua za haraka zichukuliwe kwa watendaji ambao ni wazembe ndani ya shirika hilo ikiwa ni pamoja na kuwajibishwa.


Waziri Makamba ametoa maagizo hayo Leo wakati alipotembelea kituo   cha kupoza umeme cha mkoani Arusha kilichopo Njiro jijini hapa kukagua hali ya upatikanaji wa umeme mkoani hapa kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu kukatika kwa umeme Mara kwa Mara.


Akizungumza na wanahabari Mara baada ya kukamilisha ziara hiyo Makamba alisema kwamba ifikapo Febuari 2 mwaka huu ateuliwe msemaji mpya wa shirika hilo.


"Ninaelekeza msemaji abadilishwe ifikapo febuari 2 mwaka huu achaguliwe mpya " alisema Makamba


Waziri Makamba alisema kwamba kumekuwa na changamoto kwa Tanesco kuwasiliana na wateja pindi umeme unapokatika ghafla hali ambayo imekuwa ikipelekea malalamiko kwa wateja .


"Tanesco lazima iwasiliane na wateja wake kwa wakati hii ni changamoto umeme unapokatika hivyo ni lazima wawasiliane na wateja wao kwa wakati" alisema Makamba


Hatahivyo,alisisitiza kuwa idara nzima ya uhusiano ndani ya shirika hilo lazima ivunjwe na wawekwe watu wapya wanaoweza kuendana na kasi na uweledi ndani ya shirika hilo.


"Mnawasikia wasemaji wa vilabu vya soka vya Simba na Yanga hivi mmeshamsikia msemaji wa Tanesco?" Alihoji Makamba


Hatahivyo,Makamba alisema kuwa serikali haifurahishwi na hali ya kukatika kwa umeme Mara kwa Mara na kuitaka Tanesco kutojificha nyuma ya mgongo wa waziri.


"Hatutaki waziri wa nishati ageuke kuwa msemaji wa shirika tumewaambia menejimenti wasijifiche nyuma ya wizara " alisisitiza Makamba 


Waziri Makamba  alisema kuwa serikali inakusudia kubadilisha mfumo teknolojia  wa Luku ndani ya miezi 18 kuanzia sasa ambapo wateja watakuwa wakinunua umeme moja kwa moja kupitia simu zao za mkononi na kisha kupata umeme bila kuweka tokeni.


"Mtu ananunua umeme kupitia simu yake ya mkononi na unaingia moja kwa moja kwenye mfumo na sio kuchukua tokeni na kwenda kuingiza kwenye mita" alisema Makamba


Alisema kwamba ifikapo mwezi Juni mwaka huu wateja wote takribani elfu 80  wanaosubiria kuunganishiwa umeme wataunganishiwa umeme huku akibainisha kuwa serikali inatarajia kubadilisha mfumo wa maombi ya umeme ambapo utakuwa kupitia mtandao.


Waziri Makamba alibainisha kwamba serikali inakusudia kubadili mfumo wa usambazaji wa umeme kote nchini ili uendane na kasi ya ongezeko la wateja kwa kuwa mfumo uliopo kwa sasa ni wa kizamani

Share To:

Post A Comment: