***************

Na John Mapepele- WUSM

Naibu Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Said Yakub, amesema Tamasha la Utamaduni la makabila ya Mkoa wa Kilimanjaro linalotarajiwa kufanyika Januari 22, 2022 litafungua milango ya utalii wa kiutamaduni na kuvuta wageni mbalimbali kutoka duniani kote.

Akizungumza wakati alipokuwa akikagua maandalizi ya tamasha hilo kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi, leo Januari 19, 2022 mjini Moshi amesema maandalizi yanaendelea vizuri ambapo amefafanua kwamba tamasha hilo litajumuisha sanaa mbalimbali za makabila ya Wachaga, Wapare na Wamasai.

“Tunafurahi kuona tamasha hili ni mahususi kwa ajili ya kuenzi utamaduni lakini kubwa zaidi litakuwa ni fursa ya utalii wa kiutamaduni kwani vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyakula vya kiasili, vikundi vya nyimbo, mavazi na michezo mbalimbali vitaonyeshwa siku hiyo”. Ameongeza Yakub.

Aidha, amesema Wizara inatarajia kuendelea kushirikiana na wadau katika mikoa yote kufanya matamasha kama hili ili kukuza na kuendeleza utamaduni wa makabila mbalimbali, kukuza utalii wa kiutamaduni na hatimaye kuongeza ajira na vipato.

“Msingi wa taifa lolote ni utamaduni wake, Taifa lisilo na utamaduni ni taifa lililokufa, sisi kama Wizara tutaendelea kukuza na kuuenzi utamaduni wetu kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye”. Amesisitiza Yakub

Ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kushiriki kwenye tamasha hilo ambalo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi.

Waziri mwenye thamana ya utamaduni nchini, Mhe. Mohammed Mchengerwa mara baada ya kuteuliwa hivi karibuni kuiongoza Wizara hiyo amesisitiza kuwa karibu na wadau mbalimbali wa sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanzia katika ngazi za mtaa hadi taifa ili kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta hizo.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: