Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini vimeagizwa kufanya maboresho katika utafiti,  kusimamia na kuwaandaa wataalam katika fani ya Maendeleo ya Jamii ili kuharakisha Maendeleo yanayoendana na mabadiliko ya teknolojia.

 

Dkt. Jingu amesema hayo katika Mahafali ya 12 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli, Mkoani Arusha ambapo JUMLA ya wanachuo 538 wamehitimu katika ngazi ya Stashahada na Astashahada.

 

Amesema ili kufanikiwa katika program zinazotolewa ni lazima kuzingatia dhana tatu za Uanagenzi, Ushirikishwaji Jamii na Ubunifu na Maarifa. 

 

Ameongeza kuwa Dhana  hizo zinamwandaa Mhitimu kuwa na mbinu bora zaidi katika kazi kama wataalam wa Maendeleo ya Jamii, na kumjengea  kujiajiri, kuajiriwa kuajiri wengine.

 

Dkt. Jingu amesema Wizara inatambua mchango mkubwa wa Vyuo  vya Maendeleo ya Jamii katika kuzalisha Watalaam wa Maendeleo ya Jamii wanatumika katika kuhamasisha Jamii kutatua changamoto za kimaendeleo katika maeneo yao.

 

"Naendelea kukipongeza Chuo kwa kutekeleza kwa vitendo maagizo na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali. Endeleeni kuimarisha utekelezaji wa miongozo mliyopewa ikiwa ni pamoja na kuibua nafasi zaidi kwa ajili ya wanachuo na wahitimu kujipatia ujuzi, kuendelea kutekeleza programu ya Ushirikishwaji jamii" 

 

 "Lakini pia kuwapatia wabunifu nafasi ya kuweza kuandaa kazi zao na kuwaunganisha na mitandao mingine ya kibunifu pamoja na masoko kwa ajili ya bidhaa wanazozalisha" alisema Dkt. Jingu

 

Dkt. Jingu amevitaka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii wamendelee kuimarisha utekelezaji wa miongozo waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuibua nafasi zaidi kwa ajili ya wanachuo na wahitimu kujipatia ujuzi, kuendelea kutekeleza programu ya Ushirikishwaji jamii na kuwapatia wabunifu nafasi ya kuweza kuandaa kazi zao na kuwaunganisha na mitandao mingine ya kibunifu pamoja na masoko kwa ajili ya bidhaa wanazozalisha.

 

"Nawakumbusha wahitimu na wanachuo wote kujiunga na Progamu za uanagenzi pale mnapotangaziwa, kulingana na mahitaji yenu. Programu ya hii inasaidia kutoa ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa"

 

"Ninawasihi wanachuo na wahitimu wanaopata nafasi za uanagenzi kutunza nidhamu na kujifunza kwa bidii" alisema Dkt. Jingu

 

Wakati huo huo Dkt Jingu amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya  UVIKO 19 ikiwemo kupata chanjo kwani bado upo, unaambukiza na unaua  na kuwataka kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga.

 

"Chanjo inapunguza madhara unayoweza kupata baada ya kuambukizwa ugonjwa na hivyo kuwepo kwa uwezekano wa kupona haraka. Kuna taarifa zisizo sahihi juu ya chanjo, hivyo niwasihi msikilize wataalamu wetu wa afya na Serikali." 

 

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli Elibariki Ulomi amesema Chuo kinaendelea kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia na kuiomba Wizara kuendelea kuwapatia pesa kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa kumbi pacha za mihadhara.

 

Ameongeza kuwa Chuo kinaendelea kutekeleza maagizo ya Programu za Uanagenzi na Ubunifu kwa kuwaunganisha wanafunzi na wahitimu katika Programu hizo na wanafunzi wawili wameshapata Ajira kutoka na Programu ya Uanagenzi.

 

Nao baadhi ya Wahitimu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli wamesema kuwa wako tayari kwenda kutumikia Watanzania kutokana na taaluma waliyoipata kwani wao ni Watalaam wa Maendeleo ya Jamii lazima wakaisaidie Jamii kutatua changamoto za kimaendeleo katika maeneo yao.

Share To:

Post A Comment: