Wednesday, 17 November 2021

Waziri Ummy Aagiza uchunguzi fedha za ujenzi wa Zahanati Chemka, Hai

 Na. Angela Msimbira  KILIMANJARO


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu  amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Saidi Mtanda  kuunda kamati ndogo  ya  uchunguzi  matumizi ya shilingi  milioni 50 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa Zahanati ya   Chemka,Halmashauri ya Wilaya Hai Mkoani Kilimanjaro.


Akikagua ujenzi wa zahanati hiyo leo  katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Waziri Ummy amesema hajaridhishwa na matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kiasi cha shilingi milioni 50  kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa Zahanati hiyo iliyoanza kujengwa tangu mwaka 2016 lakini hadi sasa bado ujenzi haujakamilika


“Haiwezekani Serikali ikatoa fedha  kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati hiyo, lakini bado haijakamilika   huku wananchi wakilalmika kujitoa kwa nguvu zote kuhakikisha Zahanati hiyo inakamilika kwa wakati, lakini mpaka sasa haijakamilika, hili siwezi kulivumilia, hivyo nakuagiza Mkuu Wilaya huyo kuchunguza matumizi  ya fedha hizo fedha hizo “ amesema Waziri Ummy


Ameendelea kufafanua kuwa kiasi cha shilingi milioni 25  zilitolewa na halmashauri ya Wilaya ya Hai, kupitia mapato ya ndani, wananchi walichangia kiasi cha shilingi milioni 48 huku serikali kuu   ikitoa kiasi cha shilingi milioni 50, lakini bado ujenzi huo haujakamilika jambo ambalo linawakosesha wananchi haki ya kupata huduma bora za afya na kupata huduma hiyo karibu na maeneo yao


Waziri Ummy amesema mara baada ya kupatiwa taarifa kamili ya matumizi ya fedha hizo  iwapo itagundulika kutumika kinyume na utaratibu hata sita kuwachukulia hatua wahusika wote watakaodhibitishwa  kutumia fedha hizo kinyume na utaratibu.  


Aidha , Mradi wa Ujenzi wa Zahanati ya Chemka ulianza mwaka 2016 kwa nguvu za wananchi, na ulilenga  kutatua kero ya upatikanaji wa huduma bora za afya  ambapo kiasi cha shilingi milioni 120.zimetumika ujenzi wa Zahanati hiyo.

No comments:

Post a Comment