Asteria Muhozya na Abubakari Kafumba, UAE


Ujumbe wa Wizara ya Madini ukijumuisha Viongozi na Wataalam kutoka Taasisi zake umekutana na wawekezaji wa Sekta ya Madini kutoka nchi mbalimbali wenye nia ya kuwekeza katika sekta hiyo nchini.


 Kampuni hizo ni; Elves Graphite ya Korea Kusini ambayo ina nia ya kuwekeza kwenye uchimbaji na ununuzi wa madini ya kinywe yaani graphite wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi, Kampuni ya WorldKare ya Dubai ambayo inayojishughulisha na uuzaji wa vifaa vya usalama migodini kampuni ya MCF Conseil ya Ufaransa na kampuni ya Design Fabrication India inayoshughulika na ukataji wa bidhaa mbalimbali.


Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Kampuni ya Elves Graphite Bw. Lee Jae-Jin ameeleza kuwa kampuni imepanga kuwekeza Tanzania kutokana na uhakika wa kupata walaji wa madini hayo kutoka kampuni mbalimbali nchini Korea Kusini ikiwemo ya Samsung inayotengeneza bidhaa za teknolojia.


Kwa upande wa kampuni ya MCF Conseil ya Ufaransa chini ya Rais wa kampuni hiyo Sabine Moutier, amesema kuwa wanatarajia kufanya biashara ya ununuzi wa dhahabu iliyosafishwa kutoka viwanda vya ndani. Kampuni hiyo imeomba kupatiwa taratibu za biashara hiyo ili kuweka waweze kujipanga zaidi kabla ya kuanza rasmi biashara hiyo.


Hivi karibuni, Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko ameleezea mwelekeo wa Serikali kwa siku za usoni wa kuzuia usafirishaji wa dhahabu ghafi hadi pale zitakapokuwa zimesafishwa kupitia viwanda vyake vya ndani vilivyoanzishwa katika mikoa ya Mwanza, Geita na Dodoma ambavyo vina uwezo wa kusafisha dhahabu kwa ubora wa viwango vya kimataifa.


Kwa mujibu wa Wizara ya Madini, kutokana na kuanzishwa kwa viwanda vitatu vya kusafisha dhahabu  ni dhahiri kuwa, dhahabu inayozalishwa Tanzania inaweza kusafishwa kupitia viwanda vyake hivyo kikiwemo kiwanda kikubwa katika ukanda wa  Afrika Mashariki na Kati cha Mwanza Precious Metals Refinery Limited  (MMPR) chenye  uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku katika ubora wa  kiwango cha Kimataifa cha asilimia 999.9.


Aidha, ujenzi wa viwanda vya kusafisha dhahabu nchini ni matokeo ya jitihada za Serikali kuhamasisha masuala ya uongezaji thamani madini kufanyika nchini ambapo wizara inaendelea kuvutia uwekezaji, mitaji na teknolojia za kisasa katika shughuli za madini.


Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse akizungumza na Waandishi wa Habari katika maonesho hayo amesema, kulingana na jiolojia ya Tanzania na kutokana na utajiri wa madini ya aina mbalimbali ambayo nchi imebarikiwa, ni asilimia 10 tu ya madini ambayo yameguswa huku sehemu kubwa ikiwa bado haijaguswa na hivyo kutoa wito kwa wawekezaji kuwekeza nchini kutokana na fursa zilizopo katika shughuli za madini.

‘’Tuko hapa kuvutia wawekezaji, kutangaza fursa tulizonazo lakini pia sisi STAMICO kwa niaba ya Serikali kutafuta wabia wa kuwekeza nao kwenye miradi yetu tunayoisimamia. Kama nchi tuna kila aina ya madini ambayo mengi bado hayajaguswa. Taasisi zote muhimu katika sekta zipo kwa ajili ya kuhakikisha wawekezaji wanapata taarifa sahihi na muhimu kutoka kwenye vyanzo sahihi, amesisitiza Dkt. Mwasse.


Aidha, ametumia fursa hiyo kuwatoa wasiwasi wawekezaji kutokana na mazingira mazuri ya kibiashara, usalama, kiuwekezaji, sera ambapo wataweza kufanya shughuli zao kwa amani na faida.


Amesisitiza kuwa, Serikali inachotaka ni kuona kila upande unanufaika kupitia rasilimali hiyo yaani serikali na wawekezaji.


Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Arusha Aidan Mhando ametoa wito kwa wawekezaji kufuata taratibu za kiuwekezaji kwa mujibu wa Sheria na kuzitumia Ofisi za Tume ya Madini ili kuwezesha taratibu zinazohusu masuala ya leseni na biashara ya madini kukamilishwa kwa wakati badala ya kutumia watu wa pembeni.


Taasisi za Wizara ambazo zipo katika maonesho hayo ni Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Tume ya Madini zikishirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambao ndio waratibu wa maonesho ya Expo 2020 Dubai.

Share To:

Post A Comment: