Tuesday, 23 November 2021

RC MKIRIKITI ASIKITISHWA MANISPAA YA SUMBAWANGA KUTOTEKELEZA MAAGIZO

 


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa  Joseph Mkirikiti amesikitishwa na kitendo ha Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya  kushindwa kutekeleza maagizo ya kukamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Kankwale ambayo aliyatoa mwezi Julai mwaka huu alipotembelea kijiji hicho .

Mkirikiti  amesema hayo leo wakati alipokwenda kukagua utekelezaji wa maagizo yake aliyotoa mwezi Julai kuwa Manispaa ikamilishe mradi huo ulioanzishwa na wananchi mwaka 1997 kujengwa kwa nguvu za wananchi .

" Hapa Mkurugenzi  wa Manispaa na Mstahiki Meya hamjatenda haki kwa wananchi .Mliahidi kwangu kuwa mtakamilisha zahanati hii na kuwa ilitakiwa ianze kazi mwezi Novemba mwaka huu . Hapa ni mapuuza tu yanafanyika " alisema Mkirikiti.

Mkuu huyu wa mkoa aliongeza kusema " hapa nilikuja Julai nikakuta hali hii na leo naona tena hamjatekeleza maagizo yangu. Sasa nataka Mstahiki Meya chukua hatua tuone wananchi wakiheshimika kwa zahanati hii ikamilike mwaka huu" na kuongeza kuwa hayuko tayari kushiriki uzembe wa viongozi waliopewa dhamana  kuhudumia wananchi. 

Kufuatia hali hiyo ,Mkuu wa Mkoa alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa kutumia sehemu ya fedha za ushuru wa mazao walizopokea toka NFRA  ili kukamilisha mradi huo.

" NFRA imetoa milioni 64 nendeni mkakate hiyo fedha milioni 23 leteni hapa na kukamilisha  mradi huu muhimu kwa wananchi hawa. Tupo hapa kwa ajili wananchi nashangaa wenzangu kwanini hatuwajali?" alisisitiza Mkirikiti. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa  ya Sumbawanga  Jacob Mtalitinya alisema kwa sasa zinahitajika shilingi Milioni 23 ili kazi ya kukamilisha zahanati  hiyo ikamike na kuanza kutoa huduma kwa wananchi. 

Naye Meya wa Manispaa ya Sumbawanga  na diwani wa kata hiyo Justine Malisawa alisema atahakikisha ifikapo mwisho wa mwezi huu fedha shilingi milioni 23 zinapatikana  na kupelekwa kituoni hapo .

Kufuatia hatua hiyo Mkurugenzi  huyo aliahidi kutumia fedha za ushuru wa mazao shilingi milioni 23 kati ya shilingi milioni 64 walizopokea toka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya  Chakula ( NFRA) ili wakamilishe mradi huo.

Mwananchi Nicolaus Malifedha alisema walianza ujenzi huo mwaka 1997 hadi kulifikisha kwenye renta lakini halmashauri imekua ikisua sua kutoa fedha za kukamilisha mradi huo.

"Jengo tumejenga tangu chini hadi renta lakini bado serikali imeshindwa kuchangia na kulikamilisha kama ilivyoahidi kiasi kwamba tunajiuliza kuna shetani gani ameingilia mradi huu?" alihoji mwananchi huyo.

Mkuu wa Mkoa huyo yupo kwenye ziara ya kukagua miradi ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya serikali samabamba na maandalizi ya sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment