• SAFARI yake kisiasa ilianzia mwaka 2000, alipochaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Mkuranga kwa upande wa Tanzania Bara na kisha mwaka 2005 kuhamia upande wa Zanzibar katika Jimbo la Kwahani ambalo ameliongoza kwa miaka 15.

    Huyo ni Rais wa Nane wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi. Kitaaluma, Mwinyi ni daktari wa binadamu na amepata elimu yake nchini Tanzania, Misri, Uturuki na Uingereza.

    Pamoja na kwamba ni mwanasiasa mkongwe, Dk Mwinyi anatokea katika familia maarufu kisiasa kutokana na ukweli kuwa, baba yake ni Rais wa Awamu ya Tatu, Ali Hassan Mwinyi. Dk Mwinyi, alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 baada ya kumbwaga mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalimu Seif Sharif Hamad (Marehemu).

    Kabla ya kuingia katika siasa, alitumikia kazi yake ya udaktari na mwaka 2000, ndipo alipoingia rasmi kwenye siasa na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Mkuranga (Mkoa wa Pwani).

    Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Kwahani Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alipokuwa Mbunge wa Mkuranga mwaka 2000, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afya nafasi aliyoitumikia hadi mwaka 2005, kisha akawa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) mwaka 2006 hadi 2008, Waziri wa Ulinzi Mwaka 2008 hadi 2012 na tena 2014 hadi 2020. Mwaka 2012 hadi 2014 alikuwa Waziri wa Afya.

    Dk Hussein alizaliwa Desemba 23, 1966 na kusoma katika shule za sekondari za Azania na Tambaza. Mwaka 1985 alijiunga na Chuo Kikuu cha Tiba cha Marmara huko Istanbul, Uturuki alipohitimu masomo ya tiba mwaka 1991.

    Aliongeza masomo kwenye Chuo cha Kifalme cha Tiba katika Hospitali ya Hammersmith huko London, Uingereza alipopata Shahada za Uzamili na Uzamivu (PhD), mwaka 1997.

    Miaka 1993 hadi 1995 alifanya kazi ya udaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) akaendelea kuwa tabibu na mwalimu kwenye Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Hubert Kairuki katika miaka 1998 hadi 2000.

    Rais huyo wa Zanzibar aliyetimiza mwaka mmoja tangu kuapishwa kushika wadhifa huo huku akiwa na kaulimbiu yake ya ‘Sitofukua Makaburi,’ baada ya kuchaguliwa kwake aliwaahidi Wazanzibari kuwa atalipa imani waliyompa kwa utumishi uliotukuka.

    Mwaka jana alianza safari akiwa na wanachama wenzake wa CCM zaidi ya 30 kuchukua fomu za kuwania nafasi ya kugombea Urais Zanzibar.

    Hata hivyo, baada ya mchujo majina matano yalipelekwa mbele ya vikao vya juu vya chama hicho kwa uamuzi. Katika kura za mwisho za uteuzi ndani ya chama, Mwinyi alipata kura 129 sawa na asilimia 78 ya kura zote, mshindani aliyemkaribia zaidi alikuwa na kura 19.

    Kutokana na ushindi huo wa kishindo ndani ya chama, chama hicho na yeye mwenyewe walipita katika kampeni kumnadi kuwa ni chaguo sahihi kwa Zanzibar huku akitumia kaulimbiu ya ‘Yajayo ni Neema Tupu.’

    Katika kampeni zake, alielezea vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na kupambana dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma.

    Aidha, amepania kuboresha mazingira ya sekta ya utalii ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar pamoja na kuwanyanyua kiuchumi wajasiriamali na wanawake visiwani humo.

    Novemba mwaka jana, Dk Mwinyi alitangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya Urais Zanzibar kwa kupata ushindi wa asilimia 76.27 huku mpinzani wake, Maalim Seif akiwa mshindi wa pili kwa asilimia 19.87.

    “Nimepokea ushindi kwa mikono miwili; nashukuru kuwa wananchi walio wengi wamenichagua mimi na Chama Cha Mapinduzi kwa miaka mitano ijayo.” “Nawashukuru kwa uvumilivu na ustahamilivu mkubwa.

    Niwashukuru zaidi kwa kunipigia kura… Nitalipa imani hii kwa utumishi uliotukuka,” anasema Dk Mwinyi.


    Share To:

    Post A Comment: