Na WAMJW-DSM 


WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, ameielekeza mikoa 12 iliyofanyiwa tathmini na kutakiwa kuanzisha vyumba maalumu vya kwaajili ya matibabu ya watoto wachanga itoe taaarifa yake ndani ya siku tano ili ifahamike wamefikia wapi katika jambo hilo. 


Dkt. Gwajima amesema hayo leo, wakati akizindua sehemu maalumu kwaajili ya matibabu ya watoto wachanga, uzinduzi uliofanyika katika viwanja vya hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Jijini Dar es Salaam. 


Amesema, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kudumisha huduma za afya kwa wananchi, ninaziagiza hospitali za Rufaa za Mikoa 12 zilizokidhi vigezo kutoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa jengo maalumu la matibabu ya watoto, mikoa hiyo ni pamoja na Mbeya, Ruvuma, Pwani, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Manyara, Tabora, Kagera, Mara, Dodoma na Geita.


"Nichukue fursa hii kuelekeza ile mikoa 12 niliyoitaja hapo juu kuwa ilifanyiwa tathmini na kutakiwa kuanzisha vyumba hivi, navyo itoe taaarifa yake ndani ya siku tano zijazo tujue wamefikia wapi na kama wamekwama je wamekwama wapi na wameshirikaje wadau wote kwenye maeneo yao kama walivyofanya Dar es Salaam ili kujikwamua." Amesema Dkt. Gwajima. 


Jumla ya hospitali 61 kwenye mikoa 12 ya Mbeya, Ruvuma, Pwani, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Manyara, Tabora, Kagera, Mara, Dodoma na Geita zilikidhi kuanzisha vyumba maalumu vya kutibu watoto wachanga, ikiwa ni kwa mujibu wa tathmini ya mwisho wa mwaka wa fedha 2020/202, alisisitiza Dkt. Gwajima. 


Aidha, Dtk. Gwajima amesema, Hospitali nyingine za Rufaa za mikoa zijiongeze kwa kushirikisha wadau katika maeneo yao ili kuisaidia Serikali kuboresha hudumaza afya kwa wananchi hasa hususan katika eneo la afya ya uzazi na mtoto. 


Hata hivyo, Dkt. Gwajima ameweka wazi  kuwa, Idadi ya hospitali zenye sehemu maalum kwa ajili ya matibabu ya watoto wachanga yaani NCU imeongezeka kutoka hospitali 14 Julai 2018 hadi 165 Septemba, 2021. 


Aliendelea kuweka wazi kuwa, Kabla ya ukarabati Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke ilikuwa inauwezo wa kulaza watoto wachanga 21 kwa siku ambapo baada ya ukarabati idadi hiyo imeongezeka na kufikia watoto 61 kwa siku. 


"Kabla ya ukarabati Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke ilikuwa inauwezo wa kulaza watoto wachanga 21 kwa siku ambapo baada ya ukarabati idadi hiyo imeongezeka na kufikia watoto 61 kwa siku. Amesema Dkt. Gwajima. 


Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Amana, idadi imeongezeka kutoka watoto 42 hadi 70 kwa siku, ambapo Hospitali ya Rufaa ya Mwanananyamala idadi pia imeongezeka kutoka Watoto 20 hadi 60 kwa siku, ameeleza. 


Mbali na hayo, Dkt Gwajima amesema, kuanza kwa huduma hizi kwa kiasi kikubwa kumsaidia kupunguza rufaa na msongamano wa watoto wachanga katika hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo hapo awali ndiyo ilikuwa tegemeo kubwa na pekee wa huduma za “Neonatal Care Unit”.



Hata hivyo,  amesema kuwa, taarifa zinaonesha kupungua kwa vifo vya watoto wachanga nchini kutoka 25 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2015/16  hadi 20 kwa vizazi hai 1,000 kwa mwaka 2019. 


Pia, amesisitiza kuwa, juhudi zaidi za pamoja kati ya Serikali na wadau zinahitajika katika kufikia malengo endelevu ya kufikia vifo 12 vya watoto wachanga kwa vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2030. 


Pamoja na hayo, Dkt. Gwajima ametoa rai kwa wadau wote wa afya ya mama na mtoto kuendelea na juhudi za kuimarisha  huduma za afya ya mtoto ikiwemo; uanzishaji na uimarishaji wa sehemu maalum kwa ajili ya matibabu ya watoto wachanga, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya watoto wachanga na kuwajengea uwezo watoa huduma wa watoto wachanga wagonjwa na wale wanaozaliwa na uzito pungufu. 

Share To:

Post A Comment: