Sunday, 7 November 2021

ASILIMIA 97.2 YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA HUTOKANA NA KUTOKUFUATA KANUNI BORA ZA LISHE Na.Vero Ignatus.Arusha


Tafiti za wataalamu wa masuala ya afya na lishe bora zinabainisha kuwa asilimia 97.2 za viashiria vya magonjwa hayo yanatokana na kutozingatia kanuni bora za lishe,huku Mkoa wa Dodoma ukitajwa kuongoza kwa 42.27%,ikifatiwa na mkoa wa Geita 39.94 na Arusha 38.6%.

Dkt Omari Ubuguyu ni Meneja Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya anabainisha kuwa Serikali imeendelea na mpango wake kwa vitendo Katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ambukiza ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalam zaidi ya 200 kwa lengo la kwenda katika kuhudumia jamii kwa kutoa elimu kuhusu magonjwa haya yasiyo ambukiza.

"Miongoni Mwa afua ambazo zimekuwa zikisaidia kwa Kasi kubwa Katika Mapambano haya ni pamoja na kufanya mazoezi miongoni mwetu,kwani mazoezi yamekuwa yakisaidia sana,hivyo Ukifanya mazoezi,ukizingatia kanuni za Lishe na kuachana na matumizi ya tumbaku na pombe uhakika wa kujilinda na magonjwa haya ni uhakika,Alisema Dkt Ubuguyu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela alisema Kauli mbiu ya wiki ya Magonjwa yasiyo ambukiza imebeba Ujumbe mzito kwa jamii na kuwataka kuendelea kutumia afua zinazo pendekezwa na wataalam wa afya.

"Badili Mtindi wa Maisha Boresha Afya yako" kauli mbiu hii iwe Chachu ya kukabiliana na magonjwa haya yasiyo ambukiza ili tuwe na Taifa lenye watu imara kiafya kwa ajili ya shughuli za uzalishaji,kwa uchumi wa Taifa hili,hivyo mazoezi ni miongoni mwa mambo ya msingi,tupunguze kula chumvi na sukari nyingi katika Lishe zetu"Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Wataalamu wa afya nao ni miongoni mwa wadau muhimu Katika Mapambano haya Dkt Rose Mende ni miongoni mwa madaktari bingwa wa Magonjwa ya Figo anabainisha kuwa mfumo hasi wa ulaji kwa walio wengi tangu ngazi ya familia ni miongoni mwa sababu zinazo pelekea kuongezeka kwa Idadi ya waathirika wa Magonjwa yasiyo ambukiza nchini.

Kando na hilo,kwa upande wake Afisa Lishe Prosper Mushi ambaye ni miongoni wawezeshaji kuhusu elimu hiyo anatumia jukwaa hilo kusisitiza matumizi ya Lishe bora na kujiepusha kula vyakula vyenye mafuta mengi suala ambalo huatarisha afya ya mlaji.

Juma la Magonjwa yasiyo ambukiza limezinduliwa rasmi na Naibu Waziri wa utamaduni na michezo Paulina Gekul,Jiji Arusha ambapo kilele chake ikitarajiwa kuwa Novemba 13 huku viongozi mbalimbali wakitarajiwa kushiriki akiwemo Waziri wa afya Dkt Dorothy Gwajima, ikiwa ni sehemu ya kampeni maalumu ya kupiga vita magonjwa yasiyo ambukiza nchini.

No comments:

Post a Comment