Julieth Ngarabali,


Chalinze.  Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Ummy Mwalimu amesema  Serikali imeshatoa maelekezo kwa wakurugenzi wa Halmashauri na miji nchini kuhakikisha wanaweka miundombinu rafiki kwenye majengo yote yanayojengwa kwa ajili ya mahitaji ya watu wenye ulemavu wakiwemo wanafunzi mashuleni


Amesema maelekezo hayo yametolewa kwa kutambua kuwa wapo wa Tanzania wakubwa kwa watoto ambao wanahitaji kupata huduma stahiki sawa ilivyo kwa wengine wasio na ulemavu wakiwemo wanafunzi mashuleni.


Waziri Ummy ametoa ufafanuzi huo alipokua akijibu maombi ya mwanafunzi Iddi Abas (pichani)  wa Chalinze ambaye alieleza kero ya watu wenye ulemavu hasa wanafunzi ni pamoja na miundombinu isiyorafiki ikiwemo vyoo na uhaba wa madarasa changamoto ambazo zimekuwa zikisababisha washindwe kwenda shule hivyo kuomba ifanyiwe kazi


"Mheshimiwa waziri naomba Serikali itufikie zaidi na sisi watoto wenye ulemavu tunapenda kusoma, lakini hakuna miundombinu rafiki kwenye shule nyingi , mfano mimi ninatumia baiskeli ya miguu mitatu nikifika shule inanibidi nishuke nitafute namna ya kuingia darasan, au chooni natambaa juu ya maji machafu maana baiskel haiingii sasa wengine wanaona bora wabaki nyumban"amesema Idd


Ummy amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu itafanya mabadiliko makubwa na ya tija katika sekta ya elimu  na ndio maana pia inataka Watoto wote wanaoingia kidato cha kwanza kuanzia mwakani waanze shule siku moja na sio kusubiri madarasa yajengwe kitendo ambacho wanakuja kukuta waliowatangulia wapo mbali kimasomo .


Waziri huyo amesisitiza kuwa elimu bila malipo itaendelea chini ya Rais Samia ambapo watoto wa shule za msingi na sekondari wataendelea kupata elimu bila kulipa ada ambapo  tayari zaidi ya sh. Mil . 45 zimepelekwa Chalinze kwa ajili ya shule za msingi na zaidi ya sh. Mil 100 kwa ajili ya shule za sekondari.


Aidha Ummy ameahidi kupeleka sh. Mil 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwenye shule ya msingi Chalinze ili watoto wote wenye ulemavu  wanaopaswa kuanza elimu ya msingi wapate masomo wakiwa hapo hapo na pia ameahidi kutoa sh. Mil 40 za ukamishaji ujenzi wa madarasa mawili eneo hilo.


Awali mwalimu wa shule ya msingi Chalinze inayohudumia pia watoto wenye ulemavu, Fedilia Kilambo alisema wanahudumia wanafunzi wenye ulemavu aina tofauti wakiwemo wasioona, wa viungo na akili katika darasa moja kutokana na uhaba wa majengo.


Kilambo amebainisha wanafunzi hao wanatoa maeneo mbalimbali ikiwemo Bwilingu, Chahua, Pingo na Chalinze .

Share To:

Post A Comment: