Wednesday, 6 October 2021

WAZIRI NDAKI ATATUA KERO YA WAFANYABIASHARA WA DAGAA


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na uongozi wa mkoa wa Songwe baada ya kusomewa taarifa ya mkoa ambapo amezitaka Halmashauri zote nchini kutokutumia chanjo za mifugo kama chanzo cha mapato ya Halmashauri badala yake wanatakiwa watoe huduma kwa wafugaji kulingana na maelekezo ya wizara. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Cosmas Nshenye.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wananchi wa Tunduma ambapo amewataka maafisa uvuvi kuacha kuwatoza ushuru wa usafirishaji wa mazao ya uvuvi nje ya nchi wafanyabiashara wa dagaa wa mikoa ya Songwe na Mbeya ambao hawasafirishi mazao hayo nje ya nchi.

.............................................................................

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka Maofisa Uvuvi kuacha kuwatoza ushuru wa kusafirishia mazao ya uvuvi nje ya nchi wafanyabiashara wa dagaa wanaofanya biashara hiyo kwa lengo la soko la ndani ya nchi kwenye mkoa wa Songwe.

Ametoa maagizo hayo wakati akiongea na wafanyabiashara wa dagaa katika mji wa Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe akiwa katika ziara yake ya siku mbili, ambapo wafanyabiashara hao wamedai kuwa wamekuwa wakitozwa ushuru huo wakati baadhi yao hawasafirishi dagaa nje ya nchi.

Waziri Ndaki alisema wafanyabiashara wanaopaswa kutozwa ushuru wa usafirishaji wa mazao ya uvuvi nje ya nchi, ni wafanyabiashara wa dagaa ambao hununua na kuuza kwenye masoko yaliyopo nje ya Tanzania ambapo kwa Tunduma huuzwa zaidi nchi za Zambia na Congo. Hivyo aliwataka maafisa uvuvi kuacha kuwatoza ushuru huo wafanyabiashara wanaouza dagaa kwenye soko la ndani.

"Tuache mara moja kuwatoza wafanyabiashara wa dagaa ambao wanauzia kwenye soko la ndani ushuru wa kusafirishia mazao ya uvuvi nje ya nchi katika mkoa wa Songwe kwa kigezo kuwa wote wanaziuza nje ya nchi,” alisema Waziri Ndaki

Aidha, Waaziri Ndaki aliwataka wafanyabiashara hao kufanya biashara kwa kufuata taratibu zilizowekwa na pia kuacha tabia ya kutorosha dagaa kwa kutumia njia zisizo rasmi kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru. Vilevile aliwaeleza kuwa endapo mfanyabiashara atakamatwa kwa kosa la utoroshaji dagaa atanyang’anywa leseni, mzigo wa dagaa pamoja na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.

Awali Mbunge wa Jimbo la Momba, Condester Sichalwe akiongea kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Tunduma, Ernest Silinde ambaye hakuwepo kwenye ziara hiyo, alisema kuwa suala la wafanyabiashara wa dagaa katika soko la ndani ya nchi kwenye mkoa wa Songwe kutozwa ushuru wa usafirishaji mazao ya uvuvi nje ya nchini (Export Loyality) ni kero ya muda mrefu ambayo imekuwa ikiwaumiza wafanyabiashara hao pamoja na wananchi wanaonunua dagaa. Shaban Ally ambaye ni mfanyabiashara dagaa, amemshukuru Waziri kwa maamuzi aliyoyachukua ya kuondoa ushuru huo kwa wafanyabiashara wanaouza dagaa kwenye soko la ndani kwani kilikuwa ni kilio chao cha muda mrefu.

No comments:

Post a Comment