_Profesa Kikula apongeza kasi ya Katibu Mtendaji na Menejimenti_


Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2021 katika mwaka wa fedha 2021-2022, Tume imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 151.03 ikiwa ni sawa na asilimia 93 ya lengo la kipindi husika.


Mhandisi Samamba aliyasema hayo kupitia taarifa yake ya robo mwaka wa fedha 2021/2022 ya utendaji wa Tume ya  Madini aliyoiwasilisha leo katika kikao cha Tume chenye lengo la kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kwa kipindi husika.


Alisema kuwa siri ya mafanikio hayo ni pamoja na utendaji kazi wa pamoja, kupanua huduma za Tume ya Madini kupitia uanzishwaji wa Ofisi mpya za Kimadini za Mikoa katika maeneo ya Mbogwe Mkoani Geita, na Songwe; masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini 59 vilivyoanzishwa.


Akielezea mikakati ya Tume ya Madini katika kuhakikisha inavuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli la shilingi bilioni 650 lililowekwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022, alisema kuwa Tume ya Madini imebuni vyanzo vingine vya mapato ikiwa ni pamoja na migodi ya uchimbaji mkubwa, wa kati na mdogo inayotarajiwa kuanzishwa pamoja na kuimarisha usimamizi kwenye ukusanyaji wa mapato yanayotokana na madini ujenzi na viwandani.


"Kama Tume ya Madini tunaendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato yanayotokana na madini ya ujenzi na viwanda kwa njia ya mtandao (POS) ambao utatumika na wachimbaji wa madini  hayo," alisema Mhandisi Samamba.


Wakati huohuo akielezea kasi ya utoaji wa leseni za madini katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu, Kamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma alisema kuwa Tume ilipitisha maombi ya leseni za madini 5768.


Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Reuben Lekashingo akielezea mafanikio kwenye ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini alisema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, mwaka huu jumla ya mipango 95 ya ushirikishwaji wa watanzania kwenye Sekta ya Madini ilipitishwa kati ya 98 iliyowasilishwa baada ya kukidhi vigezo.


Alifafanua kuwa ongezeko la maombi yanayopitishwa limetokana na elimu ambayo imekuwa ikitolewa na Tume ya Madini kwa wadau hususan  wamiliki wa migodi na watoa huduma kwenye migodi.


Akizungumza wakati wa kuhitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alipongeza kasi ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, menejimenti na watumishi wote kwa utendaji mzuri unaoendelea kujenga taswira chanya ya Tume ya Madini.


"Kiukweli napongeza kasi nzuri mno ya utendaji wa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, menejimenti, watumishi wote kwa ujumla, mnanifurahisha mnoo, endeleeni kuchapa kazi, tutaendelea kufanyia kazi changamoto zilizopo na zitakazojitokeza" alihitimisha Profesa Kikula.

Share To:

Post A Comment: