Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Andrew Mathew (Mb), akizindua Duka la Posta Mtandaoni ikiwa siku ya kwanza ya Wiki ya Posta inayoadhimishwa kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma. Picha na: TCRA


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Kuwe Bakari akifafanua jambo mbele ya Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Andrew Mathew, alipotembelea banda la TCRA katika viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Wiki ya Posta imezinduliwa jijini Dodoma kuelekea kilele cha Siku ya Posta Oktoba 9. Picha na: TCRA


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Kuwe Bakari akiwasilisha salamu za TCRA wakati wa tukio la uzinduzi wa Duka la Posta Mtandaoni lililofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Duka hilo la Mtandaoni limezinduliwa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na TEHAMA Mhandisi Kundo Mathew katika Wiki ya Posta. Picha na: TCRA


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Kuwe Bakari akifafanua jambo mbele ya Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Andrew Mathew wakati alipotembelea banda la TCRA katika viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma katika uzinduzi wa Wiki ya Posta. Picha na: TCRA

***************************************
Jumla ya watoa huduma za Posta 119 wasajiliwa
Shirika la Posta lazindua duka-mtandao.

Na: Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imetoa jumla ya leseni 119 kwa watoa huduma za Posta nchini na kuwapongeza kwa kutoa huduma kwa kuzingatia masharti ya leseni zao.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari wakati akiwasilisha salamu za TCRA katika uzinduzi rasmi wa Duka la Posta mtandaoni (Posta Online Shop), uliofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Jabiri amebainisha kuwa TCRA wakati wote iko tayari kushirikiana na wadau wa sekta ya posta ili kuhakikisha huduma za posta zinakuwa za kisasa zinazokidhi mahitaji na matakwa ya wananchi katika zama za ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia hasa ya Habari na Mawasiliano ni fursa ya kukuza biashara.

“Ni wajibu wetu kama wadau wa sekta ya Posta kuhakikisha kwamba tunashirikiana katika mambo muhimu ambayo yanaendelea; tumependekeza kuwa na wakati wa kushirikiana na wateja wetu katika sekta ya Posta kwa warsha ya nusu siku” alisisitiza Dkt. Jabiri.

Alibainisha kuwa, watoa huduma za posta waliosajiliwa wamekuwa wakitoa huduma ndani ya nchi, Afrika Mashariki, Kimataifa na ndani ya miji katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za posta na usafirishaji wa vipeto na vifurushi zenye uhakika wakati wote.

Katika maadhimisho hayo Shirika la Posta nchini limezindua wiki ya Posta na Duka la Posta mtandaoni linalomwezesha mtumiaji kuagiza na kuuza bidhaa ndani na nje ya nchi kwa utaratibu maalum uliowekwa na shirika hilo.

Akizungumzia huduma hiyo Kaimu PostaMasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbodo alibainisha kuwa, mtumiaji wa huduma za duka la posta mtandaoni sasa hatalazimika kusumbuka kupata bidhaa anazohitaji, kwani atachagua bidhaa aipendayo kwa njia ya mtandao na Shirika la Posta litamfikishia bidhaa hiyo popote alipo duniani.

“Mjasiriamali yeyote mwenye kitambulisho cha Mjasiriamali na Mfanyabiashara yeyote aliesajiliwa anaweza kujisajili na kuweka bidhaa zake kwenye duka letu mtandaoni” alibainisha Mbodo.

Mbodo alibainisha kuwa duka mtandao hilo linatumia lugha zaidi ya Ishirini ikiwemo Kiswahili hivyo kumwezesha mnunuzi, mjasiriamali na mfanyabiashara kuuza na kununua bidhaa zake popote duniani pasina kikwazo cha lugha.

Kwa upande wake Mgeni Rasmi Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na TEHAMA Mhandisi Kundo Andrew Mathew alisisitiza kuwa ujio wa huduma za duka la Posta Mtandaoni utawasaidia wakulima, wajasiriamali na wafanyabiashara kufanya shughuli zao kisasa hatimae kuongeza tija.

“Duka la Mtandaoni tunalozindua leo ni matokeo ya ukuaji wa teknolojia; biashara mtandaoni ndiyo mwelekeo wa biashara duniani na inawezesha jamii kuhudumiwa kwa urahisi; kwa sasa wananchi hawataifuata Posta bali Posta itawafuata popote walipo” Alisisitiza Naibu Waziri Kundo.

Mpaka sasa duka hilo la mtandaoni limesajili wafanyabiashara wapatao 300 na usajili ungali ukiendelea.

Haya yanajiri kuelekea kilele cha Siku ya Posta Duniani ambayo huadhimishwa Oktoba 9 na mwaka huu Tanzania kama mwanachama wa Umoja wa Posta Duniani inaungana na mataifa mengine kuadhimisha siku hiyo jijini Dodoma.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: