Friday, 15 October 2021

RELIANCE INSUARENCE YATIMIZA NDOTO YA GAMBO, YATOA MKOPO WA MILIONI 20 KWA AKINA MAMA 100 JIMBO LA ARUSHA

Kampuni ya bima ya Reliance imetimiza ndoto ya mbunge wa Jimbo la Arusha mjini Mrisho Gambo kwa kutoa mkopo isio na riba wa milioni 20 kwa akina mama 100 wa jimbo hilo jambo ambalo mbunge huyo alikuwa akitoa ahadi ya kuwasaidia kila anapopata fursa ya kuzungumzia shida za wananchi wake.

Akikabidhi hundi ya fedha hizo mkuu wa wilaya ya Monduli Frank mwaisumbe amesema kuwa serikali imefurahi na itauenzi mpango huo kwani wanaamini ukimuunga mama mkono jitihada hizo zinakwenda kwenye mikono mingi na kundi hilo kundi muhimu hivyo wanaomba jambo hilo liwe endelevu.

 “Serikali itaendelea kuwakumbusha na kufuatilia jambo hili kujua linaendeleaje na limefikia wapi na kwa niaba ya mkuu wa mkoa tunawapongeza akina mama mliojidhatiti kuhakikisha mnatoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine lakini pia ninaomba Reliance wakati mwingine muongeze fedha hizo ili soko la akina mama hawa likawe kubwa zaidi,”Alisema Mwaisumbe.

“Kupitia hili tunaweza kupata watu wengi zaidi watakaoona umuhimu wa kuwasaidia akina mama ila niwakumbushe mkopo huu ni fedha mmeazimwa na haina riba yoyote  na unaweza kuonekana ni fedha ndogo lakini tumeona mifano mikubwa kwa watu walioanza na mtaji mdogo lakini hivi sasa wanamafanikio makubwa kwahiyo hapa ni kujituma na uaminifu wenu tu unahitajika, msimiangushe  mbunge wenu ni mtu anayependa kujishulisha na maisha ya watu anataka aone kila mtu anastawi,” Alisisitiza Mwaisumbe.

Alifafanua kuwa Gambo ni miongoni mwa watu wachache ambao wamepata nafasi hasa mwanzomwanzo na  akaonekana jimboni mbunge huyo Bunge likiisha tuu ataonekana akishulika na shida za watu kata kwa kata katika jimbo lake.

Mbunge wa Arusha Gambo alisema kuwa anafuraha kwasababu anaona ndoto ya kuwasaidia akina mama kuinua uchumi wao inaenda kutumia kwani anajua mateso na mizigo waliyonayo na anajua wakifanikiwa ni jinsi gani wataenda kusaidia familia zao na wakati mwingine anaonekana kama anapendelea lakini anajua ukimuinua mama umeinua jamii nzima.

“Nitumie fursa hii kuishukuru kampuni ya Reliance, wanafanya kazi nchi nzima kitendo cha kukubali pendekezo letu ni jambo kubwa, ninaomba msiende kuniabisha natamani kuona mfuko huu unakuwa na kuimarika zaidi ni lazima mkazilinde na kuzitunza fedha hizi ili ziwasaidie na kuwatoa sehemu moja kwenda nyingine ndio mana kupitia mpango huu mmepewa elimu,”Alisema Gambo

Alisema kuwa kwa mtu anayetaka kufanya biashara kweli kupitia fedha hizo anaweza akainuka na akafanya vizuri na kuweza kupanda hatua kwa hatua ambapo alisisitiza kuwa wakiharibu wanajiharibia wenyewe lakini wamefanya hayo yote kwasababu wanajua thamani yao hivyo wasiende kuingiza siasa kwenye fedha hizo kwani ningeamuliwa kwenda popote hivyo waonyeshe kwamba wanathamini mchango huo.

Mwakilishi wa kampuni ya bima ya Reliance Flora Makule ambaye pia Ni mkuu wa kitengo Cha fedha katika kampuni hiyo alisema kuwa kabla ya kuwapa fedha waliona ni vyema kutoa  mafunzo kwanza kwa wanawake 100 walioanza nao ambapo wamewafundisha mambo mengi mojawapo ikiwa ni kutunza na kuwa nidhamu ya fedha.

“Mfuko huu umeanzishwa kupitia ndoto ya mbunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo ambapo itakuwa na mafanikio endapo akina mama hawa watakuwa waaminifu kurudisha kwani  kampuni hiyo ina lenga kuwasaidia makundi mbalimbali bila kujali itikadi zao na lengo lao ni kuona ustawi wa Arusha,”Alisema Bi Makule.

Kwa upande wake mwenyekiti wa umoja wa wanawake mkoa wa Arusha (UWT) Jasmin Bachu alieleza kuwa wakina mama waliopewa mkopo huo Ni akina mama wa kawaida na wameona tofauti kubwa ya mbunge wao kwa kuligisa kundi kubwa na la muhimu hivyo wanamshukuru na kumbariki na wanaamini atagusa na makundi mengine.

“ Kwa maana hiyo niwaombe akina mama fedha mtayopokea ni ya mtu mmoja mmoja haina riba na kwa umoja huu tunategemea mje mtengeneze Sacco's,  mjitahidi matumizi ya fedha yaendane na mafunzo mliyopewea, mkatunze familia kwa suala la lishe kidogo baada ya kupata faida  lakini mkakuze mitaji yenu msipeleke fedha hizi kwenye vibati wala mbesi kwani mkishindwa kurudisha mtawakosesha wengine fursa,” Alisema Bachu.

Naye mbunge wa viti maalum wanawake mkoa wa Arusha Catherine Magige   alisema kuwa hategemei akina mama hao waende saluni au baa kupitia fedha hizo bali wakafanye uzalishaji ili fedha hizo zizae wapate faida na kuweza kuzirudisha ili ziwafikie wanawake wengine.

Mwenyekiti wa umoja wa wanawake wilaya ya Arusha Merry Kisaka alisema kuwa mbunge huyo ameonuesha uungwana mkubwa kwani kidogo alichonacho ameona ni vyema ashirikiane nao ili kuwainua kiuchumi hivyo wakafanye kazi na kazi hii iendelee mbele na kuwafikia wanawake wengeine.

Hata hivyo  mmoja wa akinamama aliyenufaika na mkopo huo  Mwantumu  Shabani mjasiriamali alisema kuwa Gambo amewaonyesha jambo kubwa fedha hizo ataenda kuongea kwenye mtaji wake wa kuku wa mayai na anaamini atapiga hatua kubwa kwani fedha hizo sio ndogo kwake.

Mwengi Daudi mjasiriamali soko la Samunge alisema kuwa walioanza na Gambo toka akiwa mkuu wa mkoa baada ya kuunguliwa na soko  ambapo alikuwa anauza nyanya sanduku mbili na kutokana na fedha hizo ataenda kuuza sanduku nne hadi tano na kupata faida kubwa zaidi.


 

No comments:

Post a Comment