Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisalimia na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi Mara Warwick alipofika ofisi za wizara jijini Dar es Salaam kwa ajili kufanya mazungumzo na Waziri huyo kuhusu masula ya elimu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi Mara Warwick (hayupo pichani) wakati alipofika ofisi za Wizara jijini Dar es Slaam kufanya mazungumzo kuhusu utekelezaji wa miradi ya elimu inayofadhiliwa na Benki ya Dunia

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi Mara Warwick akizungumza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) wakati alipofika ofisi za Wizara jijini Dar es Slaam kufanya mazungumzo na Waziri huyo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Viongozi wengine wa Wizara wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Mara Warwick mara baada ya mazungumzo ya pamoja yaliyohusu utekelezaji wa miradi ya elimu inayofadhiliwa na Benki ya Dunia yaliyofanyika katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam

*******************************

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameishukuru Benki ya dunia kwa kuendelea kufadhili miradi ya elimu nchini ambayo imesaidia kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu na kuongeza Ubora.

Waziri Ndalichako amesema hayo jijini Dar es Salaam alipokutana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi Mara Warwick kwa lengo la kupitia taarifa ya tathmini ya miradi ambayo inatekelezwa kwa ufadhili wa benki ya Dunia katika Sekta ya Elimu nchini, kuainisha changamoto pamoja na kujua malengo ya mbele ya elimu ili kuhakikisha elimu inatoa mchango stahiki katika kuleta maendeleo na kujenga uchumi wa nchi.

Waziri Ndalichako ameelezea baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa Mradi wa Lipa kulingana na Matokeo ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia kuwa ni kujenga Vyumba vya madarasa 10,409, matundu ya vyoo 20,507 mabweni 646, nyumba za walimu 91, majengo ya utawala 37, maktaba 49, maabara 29 na shule mpya 44.

Ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana kutokana na kutekeleza Mradi huo kuwa ni kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa wathibiti ubora wa shule kwa kujenga ofisi mpya 155 na kufanya maboresho kwenye ofisi 31 na kuwapatia magari yanayowawezesha kuzifikia shule kwa ajili ya kuzikagua.

Mradi pia umewezesha, kuimarisha mifumo ya kuchakata takwimu kwenye sekta ya elimu ambapo kwa sasa takwimu zinakusanywa moja kwa moja kutoka shuleni jambo ambalo limeongeza ufanisi katika kupata takwimu za elimu kwa usahihi. Aidha mradi pia umewezesha kuimarisha uwiano kati ya kitabu na wanafunzi.

“Kwa kweli ninamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo na nchi marafiki, matunda yake tunayaona hasa watoto wa kitanzania wanapopata elimu bora, tutaendelea kufanya kazi kwa bidii li kuhakikisha kwa pamoja tunaleta maendeleo kwa watanzania,” amesema Prof. Ndalichako.

Waziri Ndalichako ametaja miradi mingine inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kuwa ni Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambapo tayari benki ya Dunia imetoa USD milioni 74 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa Mradi huo. Miradi mingine ni Mradi wa Kujenga Ujuzi kwa Maendeleo na Uingiliano wa Kikanda katika Afrika Mashariki (EASTRIP) wenye lengo la kuongeza fursa na ubora wa program za mafunzo ya ufundi stadi, Mradi wa Kukuza na Kuendeleaza Ujuzi (ESPJ) pamoja na Mradi wa HEET ambao utekelezaji wake unakwenda kuanza ukilenga kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika Vyuo Vikuu ili viweze kuchangia katika kukuza uchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi Mara Warwick amesema wapo tayari kuendelea kufadhili miradi ya elimu ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na kuipongeza Serikali kwa kutimiza vigezo vilivyowezesha vya Mradi wa Elimu ya Juu kwa mabadiliko ya kiuchumi (HEET) kuanza utekelezaji.
Share To:

JOHN BUKUKU

Post A Comment: