WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais wa awamu ya sita Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwatumikia, kuwahudumia na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi kwa ajili kuboresha maendeleo yao.

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Samia anataka kuona kila Mtanzania anapata huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya, elimu, maji, nishati ya umeme na miundombinu katika maeneo yao ya makazi.

 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Septemba 24, 2021) wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Ndungu wilayani Same, Kilimanjaro baada ya kukagua maboresho ya kituo cha Afya cha Ndungu akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.

 

“Wajibu wetu sisi wasaidizi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kutekeleza maelekezo ya Rais Mheshimiwa ambaye anataka kuona huduma za kijamii zikiwafikia Watanzania. Tumejipanga na tutahakikisha huduma mbalimbali zinaendelea kuimarishwa na kuboreshwa zikiwemo za afya.”

 

Mheshiwa Majaliwa amesema ujenzi wa miradi ya vituo vya afya nchini umeboreshwa ambapo kwa sasa vinauwezo baada ya kujengwa majengo ya kutolea huduma za upasuaji, mama na mtoto, maabara, wodi za kulaza wanaume na wanawake pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti.

 

Amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia Machi, 2021, Rais Mheshimiwa Samia ametoa shilingi bilioni 3.74, ambapo Julai, 2021 ameongeza tena shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya kuimarisha vituo vya afya, zahanati, ununuzi wa madawa na vifaa tiba mkoani Kilimanjaro.

 

Pia, Waziri Mkuu amewataka wakazi wa maeneo hayo waendelee kushirki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kilimo cha .zao la mpunga na mkonge. “Ninyi ni wachapakazi, kilimo cha mkonge kinalipa, nimeona mkenge unastawi vizuri huku, limeni mkonge mpate pesa.”

 

Akiwa katika Kituo cha Afya cha Ndungu, Waziri Mkuu alipokea taarifa ya maboresho ya kituo hicho iliyowasiliwa na Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Dkt. Tatizo Mwakatuya ambaye pamoja na mambo mengine alielezea changamoto zinazokikabili kituo hicho ikiwemo ya upungufu wa madaktari pamoja na jokofu la kuhifadhia maiti.

 

Kufutia taarifa hiyo, Waziri Mkuu alimuelekeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima ahakikishe daktari wa upasuaji anapelekwa haraka kituoni hapo kwani kwa sasa kituo hicho kina daktari mmoja tu wa upasuaji. Pia alielekeza lipelekwe jokofu la kuhifadhia maiti.

Share To:

Post A Comment: