KUFUATIA vurugu zilizozuka katika Kijiji cha Melela Kata ya Chita Wilaya ya Kilombero Morogoro, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigela na Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi wamefika na kuzungumza na wananchi na kufanikiwa kumaliza mgogoro wa ardhi ulikuepo.


Mgogoro uliokuepo ni wa kugombea ardhi baina ya mmiliki wa eneo la ekari 2,000 ambaye ni Gavana wa zamani wa Benki Kuu, Daud Balali na wananchi wa Kijiji hicho.


Mgogoro huo ndio uliosababisha mapigano kati ya wanakijiji na wataalamu wa ardhi wa Kanda na Mkoa ambapo wananchi hao walifanya uharibifu wa kuchoma gari, pikipiki na mali nyingine za wataalamu hao ambao walikwenda kupima ardhi hiyo.


Baada ya kutokea mapigano hayo RC Shigela na Mbunge Kunambi walifika katika eneo hilo na kusikiliza pande zote mbili na kisha kufanya maamuzi ambayo yalishangiliwa na Wananchi hao.


"Nimesikiliza pande zote mbili, siungi mkono wanakijiji waliofanya uharibifu wa mali za umma hao wote wakamatwe na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria, kuhusu eneo hili niagize mmiliki wake kusimamisha shughuli zake zote, lakini pia wataalamu wa Serikali nao wasimamishe shughuli zao za upimaji kwa muda hadi tutakapoamua vinginevyo.


Kwa hatua ya sasa niwatake wananchi wote kuwa watulivu, muendelee na shughuli zenu kwenye eneo hili kwa amani lakini mtoe ushirikiano wa kusaidia Jeshi la Polisi kuwapata wale wote waliohusika na vurugu hizi na kusababisha uharibifu wa mali," Amesema Shigela.


Awali akizungumzia ugomvi huo, Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi amesema makubaliano ya mkataba baina ya mwekezaji huyo na wananchi hao uliofanyika mwaka 2001 ulikua ni kumkabidhi Balali shamba hilo lenye ekari 2,000 kwa masharti ya yeye kuwajengea Hospitali, Shule na miundombinu ya barabara wananchi jambo ambalo kwa kipindi chote cha miaka 20 halijatekelezwa.


"Mhe RC mwekezaji huyu hajawahi kulima tangu apewe shamba hili wala hajapaendeleza na zaidi  ameenda kinyume na makubaliano aloyoingia na wananchi 2001," Amesema Mbunge Kunambi.


Baada ya maamuzi hayo yaliyofanywa na RC Shigela wananchi hao waliwapongeza viongozi hao kwa kufika kujionea changamoto hiyo ya muda mrefu huku wakiwaahidi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuwapata watuhumiwa waliochoma mali hizo za Serikali.


Tayari Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kupitia kwa Kamanda wake wa Mkoa, Fortunatus Musilim amethibitisha kuwa wanawashikilia watu sita kwa tuhuma mbalimbali za kuchoma moto mali za serikali ikiwemo Gari aina ya Land Cruiser, Pikipiki tatu, Kompyuta Mpakato na vifaa vingine vya kupimia ardhi.






Share To:

Post A Comment: