Kaimu Afisa Tarafa ya Ikungi Yahaya Njiku akizungumza kwa niaba ya Mkuu  wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hadhara Tukufu ya Mazazi ya Mtume Mohammad (S.AW) iliyofanyika Issuna  Wilaya ya Ikungi mkoani hapa jana ambayo iliandaliwa na  Jumuiya ya Kinamama wa kiislamu wilayani humo (JUWAKITA)

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro, akizungumza na Waislamu mkoani hapa kupitia hadhara hiyo.
Katibu Mkuu Baraza Kuu la Waisalamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida Sheikh Burhan Mlau, akizungumza kwenye hadhara hiyo.
Shekhat wa Mkoa wa Singida Zeana Salum, akizungumza kwenye hadhara hiyo
 Hadhara hiyo ikiendelea.
Viongozi wakiwa meza kuu.
Kaimu Afisa Tarafa ya Ikungi Yahaya Njiku, akiteta jambo na Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro  kwenye hadhara hiyo.

Mdau Shabani Mukee (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu Baraza Kuu la Waisalamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida Sheikh Burhan kwenye hadhara hiyo.



Na Dotto Mwaibale, Ikungi


MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge amewaomba wananchi mkoani hapa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya kujikinga na janga la wimbi la tatu la ugonjwa wa virusi vya Corona.

Ombi hilo limetolewa na Kaimu Afisa Tarafa ya Ikungi Yahaya Njiku kwa niaba ya Dkt.Mahenge ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hadhara Tukufu ya Mazazi ya Mtume Mohammad (S.AW) iliyofanyika Issuna  Wilaya ya Ikungi mkoani hapa jana ambayo iliandaliwa na  Jumuiya ya Kinamama wa kiislamu wilayani humo (JUWAKITA)

"Tumuunge mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kujitokeza kupata chanjo hiyo ambayo aliizindua kwa kuchanjwa na kufuatiwa na viongozi wengine mbalimbali ambapo hapa mkoani kwetu itaanza kutolewa wakati wowote katika vituo vilivyoainishwa kwenye wilaya zote,". alisema Njiku.

Akizungumza na wakina mama hao Njiku alisisitiza kuzidi kuwa wacha Mungu na kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali ili waweze kuinuka kiuchumi bila kusahau kuvaa mavazi ya stara ya kiislamu.

Aidha Njiku aliwahimiza wakina mama hao kuishi vizuri na waume zao na kuzingatia haki za ndoa na kutunza familia zao.

Njiku alipongeza ushirikiano uliopo baina ya Serikali na taasisi za dini jambo lililosaidia kuimarisha amani na mshikamano kwa wananchi kote nchini.

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro amewaomba waislamu mkoani hapa kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa wa corona hasa huu wa wimbi la tatu ambao umeelezwa kuwa ni mkali kuliko wa awamu ya kwanza na wa pili.

Nassoro aliwataka waislamu kuendelea kumuomba Mungu kuwaepusha na ugonjwa huo na kueleza wasifanye mzaha katika jambo hilo.

Alisema Tanzania bado tuna fursa kubwa kutokana na kutokuwepo kwa zuio la kutotoka nje kutokana na janga ili la Corona kama ilivyo nchi zingine ambazo wananchi wake wanashindwa hata kwenda kuswali.

Shekhat wa Mkoa wa Singida Zeana Salum alisema jumuiya hiyo ya akina mama katika  wilaya hiyo imejiwekea mikakati ya kutembelea kata zote 28 na kuwa hadi sasa wametembelea kata 18 huku wakihamasisha kuwepo kwa madrasa za akina mama na watoto katika kila msikiti.

Katika hadhara hiyo walifanya harambee ili kupata fedha za kujenga ofisi yao ya wilaya ambapo walimuomba mkuu wa mkoa awasaidie ambapo mahitaji ya kukamilisha ujenzi huo  ni Sh.19,675,000. 

Share To:

Post A Comment: