Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Bashungwa akizungumza |
Na John Mapepele, WHUSM
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana
na Wizara ya Afya leo Agosti 28, 2021 imeratibu zoezi la hiari la siku
mbili kwa timu za Taifa za michezo na wadau wote wa michezo upatiwa chanjo ya
Uviko-19 jijini Dar es Salaam ili kujikinga na ugonjwa huo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent
Bashungwa amesema makundi hayo yamependekezwa kupewa kipaumbele kwa kuzingatia,
pamoja na mambo mengine, umuhimu wao kwa jamii na ukweli kwamba kwa mazingira
ya kazi zao, wako katika hatari ya kuambukizwa.
“Ninapenda tena leo
kuendelea kusisitiza na kuhamasisha wanahabari, wanautamaduni, wasanii na wanamichezo
wenzangu kuendelea kupata huduma ya chanjo. Sekta zetu zinahudumia wananchi na hivyo
kulazimika kukutana na makundi ya watu mara kwa mara. Kutokana na hivyo tuna hatari
kubwa ya kuambukizwa, ama sisi wenyenyewe au kuambukiza wananchi ambao ndio
wadau wetu wakubwa tunaowapa huduma. Kwa vyovyote vile ni lazima tujikinge
lakini pia tuwakinge wadau wetu”. Amefafanua Mhe. Bashungwa
Amesema ili kufanikisha
zoezi hilo vimefunguliwa vituo maalum ndani ya uwanja wa Mkapa na Uhuru vitakavyokuwa
vikitoa huduma ya chanjo hiyo kuanzia saa 3 asubuhi kwa siku zote mbili ili kutoa fursa kwa wadau wote kupata huduma
ya chanjo.
Ameushukuru Uongozi wa Klabu ya Simba kwa kuwapa chanjo
wachezaji wao.
Aidha, amepongeza Klabu ya Yanga
ya kutumia wiki yao ya wananchi kuhamasisha na kupata chanjo na kulifanya zoezi
hilo la uchanjaji kuwa miongoni mwa shughuli zao muhimu watakazo zifanya siku
hiyo ambapo pia ametoa wito kwa vilabu vingine vya soka nchini kuhamasika na
kuwapatia chanjo wachezaji na watumishi wao.
Mkurugenzi wa Michezo nchini
Yusuph Singo Omary amemhakikishia Mhe. Waziri
kuwa maandalizi yote ya zoezi la chanjo yamekamilika na tayari wadau mbalimbali
wa michezo wamepongeza hatua ya Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo kuendelea kuwapa kipaombele wadau ili wajikinge.
Ametoa wito kwa Wasanii, Wanahabari na Wachezaji kwa hiari
yao kujitokeza na kutumia fursa hii kipata chanjo ili kujikinga
na kuwakinga wengine na ugonjwa wa UVIKO 19
|
|
Post A Comment: