Wanafunzi 4,105 wamechaguliwa kujiunga kidato cha tano kwa mwaka huu katika uchaguzi wa awamu ya pili kutokana na waliochaguliwa awamu ya kwanza kutoripoti kwenye shule walizopangiwa.

Hayo yamesemwa  na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Prof.Riziki Shemdoe, wakati akitangaza  matokeo ya uchaguzi wa awamu ya pili mbele ya waandishi wa habari  jijini Dodoma.

Prof. Shemdoe amesema kuwa kati ya wanafunzi waliochaguliwa, wanafunzi 499 (wavulana 424 na wasichana 75) wamepangiwa tahasusi za Sayansi na Hisabati na wanafunzi 3,604 wakiwemo wavulana 3,461 na wasichana  143 wamepangiwa tahasusi za masomo ya Sanaa na Biashara.

Amebainisha kuwa upangaji wa awamu ya pili umefanyika baada ya Wizara kujiridhisha na nafasi zilizo wazi  katika shule ambazo wanafunzi hawakuripoti.
 
==>>BOFYA HAPA KUTAZAMA MAJINA YA WALIOCHAGULIWA AWAMU YA PILI

“ Kwa kuangalia idadi ya wasichana waliopangiwa kujiunga na kidato cha tano awamu ya pili imekuwa ndogo, hii ni  kwa sababu katika uchaguzi wa awamu ya kwanza wanafunzi wote wasichana waliokuwa na vigezo walichaguliwa hivyo hapakuwa na wanafunzi wasichana  waliokuwa wamebakia,”amesema Prof. Shemdoe

Amefafanua kuwa wanafunzi wasichana waliochaguliwa katika  awamu ya pili ni wale ambao waliomba kubadilishiwa machaguo yao kutoka vyuo mbalimbali walivyokuwa wamechaguliwa awali na kupelekwa kidato cha tano.

“Wanafunzi waliopangwa awamu ya pili wanatakiwa kuripoti katika Shule walizopangiwa kuanzia  tarehe 16 hadi 30 Agosti, 2021, hivyo mwanafunzi ambaye atashindwa kuripoti hadi tarehe 30 Agosti, 2021 atakuwa amepoteza nafasi yake,”amesisitiza Prof . Shemdoe.

Aidha, amewaomba wazazi na walezi waelewe kwamba hakutakuwa na nafasi yoyote ya wanafunzi hawa kubadilishiwa shule kwa kuwa shule walizopangwa ni zile zilizobainika kuwa na nafasi kwa tahasusi husika.

==>>BOFYA HAPA KUTAZAMA MAJINA YA WALIOCHAGULIWA AWAMU YA PILI

Share To:

Post A Comment: