Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Stella Joel. 


Dotto Mwaibale, Arusha  


WANAMUZIKI wa Watanzania wanatarajia kuanza Maadhimisho ya Kimataifa  ya Muziki Duniani yatakayo zinduliwa rasmi kesho kutwa Septemba 1, 2021 jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Stella Joel alisema kesho kutwa yatazinduliwa rasmi maadhimisho hayo na kuwa mwezi Septemba wote Wanamuziki wa kada zote watashiriki kuhamasisha shughuli mbalimbali za  maendeleo.

"Kwa Dar es salaam Wanamuziki watakutana Makumbusho ya Taifa iliyopo Posta kuanzia Saa 4 asubuhi ambao watakuwa na jumbe mbalimbali za Kuhamasisha maendeleo ya muziki na kushiriki shughuli za ujenzi wa Taifa," alisema Joel.

Joel alisema kwa upande wa Arusha Wanamuziki watakutana katika Makumbusho ya Taifa na kwa Mkoa wa Mwanza  watakutana na Kufanya ziara ya Utalii wa Ndani na  kujionea vivutio vya utalii wa nchi yetu na kukitangaza Kisiwa cha Sanaane.

Alisema wamechagua Jiji la Arusha kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa maadhimisho hayo  Kimataifa kwa sababu Mkoa wa Arusha upo katikati ya Afrika pia una Historia kubwa ya nchi yetu ambapo Mhasisi wa Taifa letu Hayati Mwalimu Julius Nyerere alianzisha Azimio la Arusha katika mkoa huo na alitembea kwa miguu na viongozi wengine kuunga azimio hilo na kuwa  Arusha ndipo kilipo kiti na mti wa Mwalimu  Nyerere.

Alisema kesho kutwa Wanamuziki watakutana Makumbusho ya Azimio la Arusha kuanzia Saa 4 asubuhi na kuhamasisha shughuli za maendeleo na kufanya Utalii wa Utamaduni katika jiji la Arusha.

Joel alitumia nafasi hiyo kuwaomba wanamuziki wote katika maeneo hayo kujitokeza kwa wingi ili kukamilisha jambo hilo.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: