Na Elizabeth Joseph, Monduli.


MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeshauriwa kuangalia namna ya kuimarisha afya za walengwa wao kutoka Kaya masikini katika Awamu ya tatu kipindi cha pili kupokea mradi kwa kuwaunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii(CHF).


Ushauri huo ulitolewa Jana Na Mkuu wa Wilaya ya Monduli Frank Mwaisumbe wakati akifungua Kikao kazi TASAF chenye lengo la kujenga uelewa kuhusu mpango wa TASAF kipindi Cha pili kilichowahusisha Viongozi,Watendaji na Wawezeshaji wilayani humo.


Alisema kuwa suala la kuimarisha afya za walengwa wao katika mradi huo ni la msingi na linafaa kupewa mkazo ili kusaidia wanufaika hao kukuza uchumi wao wakiwa na afya njema.


"Ni kweli tunahitaji hizi familia zikue kiuchumi lakini watawezaje kukua kiuchumi kama afya zao sio nzuri?"alihoji Mwaisumbe


Aliongeza kusema kuwa katika Wilaya yake zipo Kaya zaidi ya 36,000  ambazo hazina uwezo wa kupata matibabu hivyo hali hiyo inaweza kusababisha fedha za mradi wa TASAF kutumika kwenye matibabu na sio kutumia kwa malengo waliyokubaliana.


"Hawa watu wangekuwa na Bima ya Afya hiyo 30,000 maana yake wangeweza kutumia gharama ndogo ya matibabu kwa mwaka mzima hivyo nasisitiza kwamba pamoja na kuwawezesha wananchi wetu kiuchumi lakini pia tufikirie jamii kuhusu afya zao"alisema Mkuu huyo.


Naye Ofisa Miradi wa TASAF Makao Makuu Henry Mbago alieleza kuwa Awamu ya pili ya mradi huo imekuja na teknolijia mpya ya kutumia Kishkwambi(Tablet) katika kuhakiki taarifa za walengwa na kusema kupitia teknolijia hiyo wanaamini watapata walengwa wenye sifa zinazotakiwa.


"Mwezeshaji atafika kwenye Kaya husika iliyoibuliwa na wananchi wenyewe, teknolijia hii itaonesha majira nukta(GPS) na kupiga picha ya hiyo Kaya"alisema Mbago.


Aidha alibainisha kuwa katika kipindi cha kwanza Awamu ya tatu ya TASAF takwimu zimeonesha kuwa umasikini wa mahitaji ya msingi kwa Kaya za walengwa umepungua kwa asilimia 10 huku umasikini uliokithiri kwa Kaya za walengwa ukipungua kwa asilimia 12 na kusema mafanikio hayo yametokana na walengwa kujikita katika shughuli za kukuza kipato na kujiimarisha kiuchumi.


Kwa Upande wake Ofisa Ufuatiliaji TASAF Makao Makuu Jesma Ponela alisema Awamu ya pili ya mradi huo itafikia vijiji vyote 32 wilayani humo ambavyo havikufikiwa katika Awamu ilitopita hivyo kuwataka Wawezeshaji kuishirikisha Jamii husika katika kubaini Kaya masikini ili kutoleta malalamiko hapo baadaye.


Awali Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli Isack Kadogoo aliwataka viongozi hao kuzingatia viapo wanavyoapa katika kutekeleza majukumu yao kwa kutenda haki bila kuwa na upendeleo ili kuonesha uzalendo kwa watanzania.


"Unapokula kiapo Cha kutenda haki wengi tunasahau kuwa tunajilaani wenyewe kwa kutotenda haki,hatukumbuki kile kiapo Sasa naomba tuzingatie viapo tunavyoapa kwa kuhakikisha tunapata walengwa"aliongeza Kadogoo. 


Share To:

Post A Comment: