Na Mariane Mariane Mgombere, Busega-Simiyu.

Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amezindua rasmi zoezi la chanjo ya UVIKO 19 (COVID 19) Wilayani Busega, uzinduzi uliofanyika Hospitali ya Wilaya ya Busega, huku akiwataka wananchi kupuuza maneno na taarifa za kizushi zinazoendelea kusambaa kwenye baadhi ya Mitandao kuhusu chanjo hiyo. Mhe. Zakaria amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata chanjo, kwani Serikali ina malengo mazuri katika kupambana na ugonjwa huo.

Aidha, Mhe. Zakaria amesema ni muhimu kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo ili kupunguza maambukizi ya UVIKO 19.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu Wilaya ya Busega, Dkt. Beatus Silas amesema zoezi la chanjo ya UVIKO 19 imezinduliwa rasmi siku ya tarehe 05 Agosti 2021, na zoezi litaendelea mpaka tarehe 11 Agosti 2021, huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi.

Nae, mratibu wa chanjo Wilaya ya Busega Bw. Mussa Shaban amesema Wilaya imepokea jumla ya chanjo 2875 na itatolewa katika vituo 3 vilivyoelekezwa na Wizara ya Afya, ambavyo ni Hospitali ya Wilaya, Kituo cha Afya Lukungu na Kituo cha Afya Igalukilo, hivyo wananchi waendelee kujitokeza kwaajili ya kupata chanjo hiyo.

Kwa upande wa wananchi baada ya kupata chanjo hiyo wamesema waniashukuru Seriakli kwa kuleta chanjo nchini na kusisitiza kwamba ni muhimu kwa wananchi wengine kujitokeza kuchanja ili kuwa na kinga dhidi ya ugonjwa huo, kwani chanjo hiyo haina utofauti na chanjo nyingine.

Share To:

Post A Comment: