Sunday, 18 July 2021

ZELOTHE ARIDHISHWA NA UJENZI WA NYUMBA ZA WALIMU

 Mwenyekiti wa CCm Mkoa wa Arusha Zelothe Stephen na Wajumbe wa Kamati ya siasa Mkoa wakikagua nyumba nne zawalimu zilizogharimu milioni mia moja {100}

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha Zelothe Stephen akiwa ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya siasa Mkoa wameitembelea shule ya Sekondari ya Sale iliyopo katika Halmashauri ya Ngorongoro na kukagua hatua za ujenzi wa nyumba nne za walimu zilizofikia asilimia 85% kukamilika.


Haya yamejiri wakati wa ziara yake ya kuimarisha shughuli za uhai wa Chama katika ngazi ya mashina na matawi ambapo akiwa katika Wilaya ya Ngorongoro alipita shuleni hapo kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kupitia mpango wa PEA.

Gharama  za ujenzi wa nyumba hizo inatajwa kuwa shilingi milioni  mia moja (100) ukamilishwaji wa Maabara Milioni tatu {3} pamoja na ujenzi wa vyoo vya wanafunzi matundu kumi na mbili {12} milioni 13.2 huku wananchi wa Kata za Sale ambao watoto wao wanasoma katika shule hiyo wakiunga mkono hatua hizo za ujenzi  kwa kufanya kazi za mikono kwa  kuchimba msingi,kukusanya mawe pamoja na kuchimba mashimo ya vyoo ili  walimu wa shule hiyo waendelee kuwa karibu na shule ili kuwafanya wanafunzi wafanye vizuri katika masomo yao.

Zelothe amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mwalimu Raymond Mangwala pamoja na Mwalimu Mkuu wa Sale Sekondari kwa usimamizi mzuri wa fedha za Serikali katika ujenzi wa maabara,Vyoo vya wanafunzi sambamba na Nyumba za Walimu,huku akifurahishwa na ubunifu na utendaji kazi wenye tija wa Mwalimu Mkuu huyo.

Naye Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Ngunai Gidore ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Chama cha Mapinduzi kwa kuongeza thamani ya ujenzi katika shule hiyo.

Katika ziara hiyo ya kuimarisha shughuli za Uhai wa Chama katika ngazi ya mashina Mwenyekiti wa Ccm Mkoa ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa Ndugu Robert Kaseko,Neema Mollel na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (MNEC) Dkt. Daniel Pallangyo ambapo katika shughuli ya kuimarisha Uhai wa Chama na Jumuiya wameendelea kukutana na Viongozi wa Mashina,na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM huku wakikutana na makundi mbalimbali ya Wazee,Wanawake na Vijana.

No comments:

Post a Comment