Na Mwandishi wetu, Dodoma
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imezindua Tovuti ya Wizara hiyo inayopatikana katika kikoa cha www.mawasiliano.go.tz  pamoja  Mpango Mkakati wa Wizara hiyo wa miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2025/26 ambao ni mwongozo wa utendaji kazi na upimaji wa malengo iliyojiwekea ya kuibadilisha jamii ya Tanzania kuwa yenye msingi wa maarifa ambayo yamewezeshwa kidijitali

Hafla ya uzinduzi huo imefanyika leo tarehe 1/07/2021 mjini Dodoma na kuhudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Manaibu Waziri, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso, wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara na mjumbe  kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Akifungua hafla hiyo Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Mpango Mkakati huo umejikita katika nyaraka mbalimbali za kisera na zile za malengo ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa pamoja na Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2021-2025 katika vipengele vinavyogusa masuala ya mawasiliano na teknolojia ya habari.

Alisema kuwa Wizara hiyo ina jukumu la kuhakikisha wananchi wanatumia fursa zinazoenda sambamba na maendeleo ya kidijitali kwa kuweka mazingira wezeshi ya mwananchi kupata huduma za kijamii na kiuchumi kwa njia ya mtandao mahali popote alipo

Aidha, amesema kuwa Wizara hiyo inakwenda kuandaa mpango wa uwekezaji katika uchumi wa kidijitali ambao utaelezea malengo na mikakati ya nchi katika kuipeleka nchi ya Tanzania katika  uchumi wa dijitali.

Katika hatua nyingine Mhe. Dkt. Ndugulile ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuiona Wizara hiyo ni nyenzo kuu ya uchumi na maendeleo ya nchi na kuiongezea bajeti ya maendeleo kutoka bilioni 15 hadi bilioni 246 zilizopitishwa kwa mwaka wa fedha 2021/22

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa Mpango Mkakati huo  unaenda kujibu mahitaji ya watanzania ambapo Wizara na taasisi zilizo chini yake zimejipanga vema kuhakikisha inatimiza malengo waliyojiwekea ya kuwa na jamii iliyowezeshwa kidijitali

Awali akitoa wasilisho la Mpango Mkakati huo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amezungumzia malengo ya mpango mkakati huo kuwa ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano,Teknolojia ya Habari,  na Huduma za Posta, kuimarisha uwezo wa taasisi zake katika utoaji wa huduma, kuimarisha fursa za kidijitali na kuboresha usimamizi wa teknolojia ya habari, mawasiliano ya simu na huduma za posta nchini.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Share To:

Post A Comment: