Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Selemani Jafo akiongea wakati wa Mkutano na Wadau wanaosafirisha, kuingiza na kusambaza taka hatarishi katika ukumbi wa Millenium Tower jijini Dar es Salaam, ikiwa ni kusikiliza changamoto za Wadau hao.

Sehemu ya Wadau wanaojishughulisha na biashara ya taka hatarishi. Amekutana na Wadau hao jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Millenium Tower ili kusikiliza maoni yao juu ya biashara hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Selemani Jafo akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wakati wa kikao hiko kilichokutanisha Wadau wanaosafirisha, kuingiza na kusambaza taka hatarishi.

Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt Andrew Komba akiongea wakati wa Mkutano wa Wadau wanaosafirisha, kuingiza na kusambaza taka hatarishi katika ukumbi wa Millenium Tower jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi NEMC Bi.Esnat Chaggu akizungumza wakati wa Mkutano na Wadau wanaosafirisha, kuingiza na kusambaza taka hatarishi katika ukumbi wa Millenium Tower jijini Dar es Salaam, ikiwa ni kusikiliza changamoto za Wadau hao.

**********************

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Selemani Jafo amekutana na Wadau wanaojishughulisha na biashara ya taka hatarishi. Amekutana na Wadau hao jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Millenium Tower. 

Amesema kuwa hivi karibuni kumejitokeza changamoto nyingi katika kusimamia jukumu hilo na ameona ni vyema akakutana na wadau wanaojihusisha na shughuli za kukusanya, kusafirisha, kuhifadhi, kuingiza nchini, kusafirisha nje ya nchi na urejelezaji wa taka hatarishi ikiwemo taka za kielekitroniki ili kwa pamoja kuweza kujadiliana namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo na kutoa mapendekezo na maelekezo yatakayoimarisha usimamizi na udhibiti wa taka hatarishi nchini. 
 
Aidha aliongeza kuwa  Ofisi ya Makamu wa Rais  kwa kushirikiana na wadau ilifanya mapitio na kufanya marekebisho ya Kanuni za Udhibiti wa Taka Hatarishi za Mwaka 2019 na kuandaa Kanuni mpya za Udhibiti na Usimamizi wa Taka Hatarishi za Mwaka, 2021 (The Environmental Management (Hazardous Waste Control and Management), 2019 na kufanya mapitio ya Kanuni za Ada na Tozo za Mwaka, 2019 na kuandaa Kanuni za Ada na Tozo za Mwaka, 2021.  

Pamoja na masuala mengine,  lengo kuu la kufanya mapitio ya Kanuni hizi lilikuwa ni  kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa taka hatarishi nchini. 
 
“Ikiwa ni takriban miezi miwili sasa tangu Kanuni hizi zilipopitishwa mwezi Mei, 2021 na kuanza utekelezaji wake,  nimeona ni vyema pia tukumbushane matakwa ya Kanuni hizi na nyie wadau mtueleze changamoto mnazokumbana nazo katika kuzingatia matakwa ya Kanuni husika ili sote kwa pamoja tuweze kuimarisha usimamizi wa taka hizi”.

 Pia alitumia wasaa huo kuwakumbusha Wadau hao  kuwa Tanzania imeridhia Mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda  ambayo inatoa fursa ya ushirikiano wa kimataifa katika kusimamia na kudhibiti usafirishaji wa taka hatarishi baina ya nchi na nchi.

Miongoni mwa Mikataba hiyo ni Mkataba wa Basel unaosimamia udhibiti wa usafirishaji wa taka hatarishi  kutoka nchi moja na kwenda nchi nyingine na Mkataba wa Bamako unaozuia uingizaji na usafirishaji wa taka hatarishi ndani ya Afrika ambayo yote kwa pamoja tuliridhia mnamo mwaka 1993.
 
Katika kutekeleza matakwa ya  Kanuni mpya za Udhibiti na Usimamizi wa Taka Hatarishi za Mwaka, 2021 (The Environmental Management (Hazardous Waste Control and Management), na Utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa tuliyoridhia kumekujitokeza changamoto mbalimbali. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na: Baadhi ya wadau kuingiza nchini Taka hatarishi bila kupata  idhini kutoka Mamlaka za Nchi ambayo Shehena inatopotoka na inapoingia,  Baadhi ya wadau kuchelewa kuhuisha vibali na hivyo kupelekea usumbufu katika uendeshaji na usimamizi wa shughuli za ukusanyaji, uhifadhi na usafirishaji wa Taka hatarishi,  Baadhi ya wadau kutokuwasilisha taarifa za viwango vya taka hatarishi walivyokusanya/hifadhi/kusafirisha kama inavyoelekezwa katika kanuni za taka hatarishi za mwaka 2021 (Ripoti ya kila nusu mwaka),  Baadhi ya wadau kutowasilisha nyaraka sahihi na kwa wakati na hivyo kusababisha ucheleweshaji katika utoaji wa vibali,  Baadhi ya wadau kutokufuata utaratibu katika kufuatulia vibali vyao ikiwemo kufuatilia vibali moja kwa moja Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira bila kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Baadhi ya wadau ya wadau hususan wanaojishughulisha na shughuli za ukusanyaji, uhifadhi na usafirishaji wa Chuma chakavu kuhujumu miundo mbalimbali nchini.
 
Alimalizia kwa kusema kuwa   pamoja na changamoto hizo Ofisi ya Makamu wa Rais  inatambua mchango wenu katika shughuli za udhibiti na usimamizi wa taka hatarishi ikiwemo taka za kielekitroniki  na tunafahamu kabisa dunia yote kwa sasa inaelekea kwenye uchumi wa mzunguko  ambao kwa lugha rahisi tunaweza kuuita “taka ni mali” (circular economy), kwa hiyo ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za uhifadhi wa mazingira kwa maendeleo endelevu  ni muhimu sana. 

Akiongea katika Mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka amesema kuwa Mkutano huo una lengo la kujua changamoto zinazowakuta wadau wa biashara hiyo.

Naye mmoja wa Wafanyabiashara hao kutoka Gaia Industry Bi Rehema Ally, ametoa maoni kuwa mchakato wa vibali vya taka hayarishi uanze kufanyika  mtandaoni (online). Katika suala hilo Waziri Jafo ametoa maagizo kwa NEMC  kuwa katika siku 45 mchakato huo wa mtandaoni uwe tayari umekamilika na kuwezesha Wadau kutumia mfumo huo.

Share To:

Post A Comment: