Na Munir Shemweta, WANMM KILOSA

                                           

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewajia juu na kutoa onyo kwa wenyeviti wa vijiji wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro wanaojihusisha na kuuza ardhi ya vijiji bila kufuata taratibu.

 

Dkt Mabula alitoa onyo hilo tarehe Julai 12, 2021 alipozungumza na wananchi wa kata ya Dumila wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro akiwa katika ziara yake ya kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za ardhi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara katika mkoa huo.

 

Akiwa mkoani Morogoro hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa Dumila wilayani Kilosa kuhusiana na migogoro ya ardhi waliyoieleza kuwa imekuwa ikisababisha kushindwa kuendelea na shughuli za uzalishaji mali.

 

Dkt Mabula alisema, migogoro mingi ya ardhi imekuwa ikisababishwa na wenyeviti wa vijiji hasa katika suala zima la ugawaji ardhi na kusisitiza kuwa, jukumu la kugawa ardhi ya kijiji kwa mujibu wa sheria ni mkutano wa kijiji na siyo mwenyekiti.

 

 ‘’Naomba muelewe kuwa mwenyekiti wa kijiji haruhusiwi kugawa ardhi na yeyote atakayepewa ardhi na mwenyekiti wa kijiji basi ajue imekula kwake’’ alisema Dkt Mabula.

 

Naibu Waziri wa Ardhi alimuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro Frank Minzikuntwe kuwapitisha katika sheria ya ardhi ya usimamizi viijiji wenyeviti wa vijiji ili waweze kuielewa na kusimamia vizuri ardhi katika maeneo yao.

 

"Kasimamieni vizuri vijiji vyenu na mhakikishe ardhi katika maeneo yenu inapangwa, inapimwa na kumilikishwa maana upangaji ardhi katika maeneo yenu utapunguza migogoro ya ardhi " Alisema Dkt Mabula.

 

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela alimhakikishai Naibu Waziri Mabula kuwa atahakikisha sheria za usimamizi wa ardhi katika mkoa wake zinasimamiwa vizuri ili kuhakikisha migogoro ya ardhi katika mkoa huo inapungua au inakoma kabisa.

 

Awali Dkt Mabula alianza utekelezaji maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kikao cha ndani na viongozi wa wilaya ya Kilosa kwenye ofisi ya Kata ya Dumila wilayani Kilosa na kuhusisha wenyeviti wa vijiji, watendaji wa mitaa, madiwani pamoja na wananchi waliowasilisha malalamiko kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

 

Katika kikao hicho, wenyeviti wa mitaa wakiongozwa na madiwani walimueleza Naibu Waziri kuwa, migogoro ya ardhi katika maeneo yao inahusisha mipaka kati ya vijiji, kubomolewa kwa baadhi ya nyumba za wananchi, kutopimwa baadhi ya vijiji, wananchi kuzuiwa kuendelea na shughuli za kiuchumi na wanaodaiwa wamiliki halali pamoja na mgogoro ya uvamizi wa maeneo.

 

Akieleza suala la migogoro ya mipaka, Dkt Mabula alisema, suala la kupima mipaka ni la halmashauri kwa kutenga fedha kwa ajili ya kazi hiyo na kuhakikisha vijiji vinapimwa na kupatiwa vyeti na alitaka utengaji fedha ufanyike kila mwaka.

 

"Sisi kama Wizara hatuna wajibu wa kupima mipaka ya vijiji, madiwani mtekekeze majukumu yenu kwa kusimamia upimaji vijiji na msipotekekeza kilosa haitakaa itulie na RAS aunde timu yake chini ya usimamizi wa mpima wa mkoa na kuweka kambi vinginevyo hatuwezi kufika" Dkt Mabula.

 

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wtumishi watatu wa wizara hiyo walioshindwa kuripoti katika kituo chao kipya cha kazi kwenye halmashauri ya wilaya ya Kilosa.

 

‘’Kama mtakumbuka tulifanya maamuzi magumu kwenye mkoa wa Morogoro kwa kuhamisha asilimia 90 ya watumishi wa sekta ya ardhi na wapo watumishi watatu waliopangiwa kufanya kazi hapa Kilosa lakini mpaka sasa hawajaripoti, namuagiza kamishna wa Ardhi awasiliane na  Katibu Mkuu ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao’’ alisema Dkt Mabula.
Share To:

Post A Comment: