Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (ACP) Stella Mutabihirwa, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya jeshi hilo mkoani hapa leo hii.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (ACP) Stella Mutabihirwa, akiwaonesha  waandishi wa habari (hawapo pichani) misokoto ya bangi iliyokamatwa na jeshi hilo.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida

MWANAMKE mmoja Moshi Mkimbu (40)  mkazi wa Kijiji cha Ndulungu Tarafa ya Ndago Wilaya ya Iramba  mkoani Singida ameuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali  na mume wake aitwaye Juma Shabani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (ACP) Stella Mutabihirwa akizungumza na waandishi wa habari leo  aamethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo lilitokea Julai 18, 2021 katika  kitongoji cha Misughaa na kuwa  mtuhumiwa  alikamatwa na atafikishwa mahakamani  kujibu shitaka  lake. 

Mutabihirwa alisema kuwa uchunguzi  wa  awali wa Jeshi la polisi  umebaini kuwa chanzo kikubwa cha mauaji  hayo  ni  ugomvi  wa  kifamilia  pamoja  na ulevi  baada ya  marehemu  kudai  pesa za  mahindi  yaliyouzwa  kwa  ajili ya ada ya mtoto shuleni, ndipo mume wake  huyo alianza  kumshambulia kwa kumpiga na fimbo na kitu  chenye  ncha kali na kusababisha kifo cha mke wake. 

Katika tukio lingine alisema jeshi hilo mkoani hapa linaendelea na misako mbalimbali ya kubaini uhalifu kutokana na mikakati iliyojiwekea ya kuweka mkoa wa singida salama ambapo kwa kipindi cha miezi mitatu Aprili hadi Julai 2021, Jeshi la polisi limefanya misako na kufanikiwa kukakamata dawa aina bhangi misokoto 757 watuhumiwa tisa (9), watuhumiwa saba kesi zipo mahakamani hatua ya kusikilizwa na watuhumiwa wawili wametiwa hatiana.

Alisema mtuhumiwa mmoja wa dawa za kulevya  aina heroine kete moja alikamatwa  na kesi ipo mahakamani na  Pombe ya moshi (gongo) lita 113 zilikamatwa na watuhumiwa  24   ambapo watuhumiwa walifikishwa  mahakamani.  

"Kesi 16 watuhumiwa walitiwa hatiani na watuhumiwa 8 kesi bado zinaendelea mahakamani hatua ya kusikilizwa na pia pikipiki moja aina ya SANLG ilikamatwa baada ya pikipiki hiyo kuporwa  na mtuhumiwa mmoja ambaye alikamatwa na alifikishwa mahakamani na tayari  amehukumiwa kutumikia jela mwaka mmoja," alisema.

Mutabihirwa  ametoa shukrani kwa wananchi na raia wema kwa kutoa ushirikiano na kupata mafanikio hayo hivyo  wito wa jeshi hilo kwa  wananchi  wote hususani  wanandoa  kuacha tabia na vitendo  vya  ukatili wa kijinsia katika  familia zinazo wazunguka na kuwatengemea kwani vitendo hivi hupelekea madhara makubwa  na  kusababisha  vifo  katika jamii. 

Aidha Mutabihirwa amewataka wananchi kuacha tabia ya ulevi uliopindukia na matumizi ya dawa kulevya bali waishi  kwa amani, furaha na  kufuata sheria za nchi na pindi matatizo ya kifamilia yanapotokea wafike kwenye vituo vya Polisi kwenye madawati maalumu ya kushughulikia  masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na watoto na si kujichukulia sheria 
mkononi.

Share To:

Post A Comment: