Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu, akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Sambaru wakati akiongoza harambee ya ujenzi wa Shule ya Msingi ya Kipompo iliyofanyika Kata ya Mang'onyi wilayani Ikungi mkoani Singida jana.

 Diwani wa Kata ya Mang'onyi itakapojengwa shule hiyo, Innocent Makomero akizungumza kwenye harambee hiyo.
Watoto wa Kijiji cha Sambaru wakimpokea kwa mabango Mbunge Mtaturu wakiomba kujengewa shule katika kitongoji cha Kipompo.

Watoto wa Kijiji cha Sambaru wakimpokea  Mbunge Mtaturu.
Mkazi wa Kijiji cha Sambaru Hussein Dede, akimpokea  Mbunge Mtaturu.
Matofari ya ujenzi wa shule hiyo yakifyatuliwa kwa nguvu za wananchi.
Harambee ikiendelea.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Sambaru Samsoni Mwaigaga akizungumza kwenye harambee hiyo.
Wadau wa maendeleo ya elimu ambao ni wachimbaji wadogo wa madini wakitambulishwa  na Diwani wa Kata ya Mang'onyi itakapojengwa shule hiyo, Innocent Makomero (kulia) kwenye harambee hiyo.
Makofi yakipigwa kwenye harambee hiyo
 



Na Dotto Mwaibale, Singida



ZAIDI ya 23 milioni zimechangwa na wadau mbalimbali mkoani hapa kwa lengo la kupunguza adha ya watoto wa Shule ya Msingi ya Kipompo  iliyopo Kata ya Mang'onyi, Wilaya ya Ikungi  kutembea umbali mrefu wa takribani kilomita 15 kila siku kuwahi masomo.

Akiongoza harambee hiyo, Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ambaye kati ya fedha hizo alichangia 5 milioni alisema fedha zilizopatikana  zitatumika kwa ujenzi wa madarasa manne kwenye shule hiyo inayotarajiwa kuanza kujengwa kwenye kijiji cha Sambaru kwa nguvu ya wananchi. 

Hata hivyo, Mbunge Mtaturu alipongeza juhudi za makusudi katika nyanja mbalimbali za maendeleo hasa eneo la elimu  zinazofanywa na wananchi wa kijiji hicho ambacho kina vitongoji vitatu vya Kipompo, Mbugani na Mkunguu.

"Hapa ninapozungumza tayari wananchi hawa kwa nguvu zao  wamenunua mifuko ya saruji 210 kwa hatua za maandalizi ya ujenzi wa awali bila kusubiri serikali" alisema.

Mbali ya mchango huo zaidi Mtaturu aliwatia moyo wananchi hao kuendelea na mshikamano huo kwa kuhakikisha wanasonga mbele katika kufanikisha shabaha iliyopo ya ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa na nyumba ya mwalimu, huku akiahidi kuwawezesha kumalizia hatua ya kupaua.

Mtaturu alisema wametoka kwenye Bajeti ya Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imelenga kuwaletea wananchi maendeleo. 

"Tunamshukuru sana Rais kwa kuonyesha upendo mkubwa kwa watanzania tumuunge mkono," alisema Mtaturu.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mang'onyi itakapojengwa shule hiyo, Innocent Makomero alisema kukosekana kwa shule kwenye Kijiji cha Kipompo kumeibua changamoto kadhaa ikiwemo kuzorotesha ustawi wa elimu sambamba na kuleta athari za saikolojia kwa watoto kutokana na kutembea umbali mrefu.

Alisema azma iliyopo ni kuhakikisha anaunga mkono juhudi za mbunge na wananchi katika kuhakikisha wanafanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo ya elimu.

"Ili kufanikisha jambo hili nimewaalika wadau mbalimbali wa maendeleo ya elimu wakiwemo wachimbaji wadogo wa madini kuja kutuunga mkono katika harambee yetu hii," alisema Makomero.

Mwanafunzi wa darasa la sita kwenye Shule ya Msingi Sambaru Nuru Ramadhan ambaye ni miongoni wa wahanga wa kutembea umbali mrefu akitokea kitongoji cha kipompo, alisema safari ya kutoka nyumbani alfajiri kwenda shuleni huwachukua kati ya masaa 3 hadi 4 kufika shuleni na hawajawahi kufanikiwa kuwahi vipindi vya asubuhi.

"Tunawashukuru wazazi wetu kwa uamuzi huu sababu kukamilika kwa shule hii kutasaidia  kupandisha ufaulu na kupunguza baadhi ya kero ikiwemo kushinda na njaa, na mafuriko kipindi cha mvua wakati tukiwa njiani kilomita 15 kila siku kwenda shule na kurudi." alisema.

Katika harambee hiyo jumla ya 23 milioni zilipatikana zikijumuisha fedha taslimu, ahadi na michango mingine ya hali na mali.

Share To:

Post A Comment: