Na. Steven Nyamiti, Dodoma


Waziri wa Madini Doto Biteko amezindua rasmi   Jukwaa la Wadau wa Madini  kupitia Benki ya NMB lenye lengo la kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara, wachimbaji  na wadau wa madini ili kuwa na sauti moja katika kujadili changamoto  wanazokabiliana nazo  na kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja.


Hafla ya Uzinduzi wa Jukwaa hilo  unaokwenda kwa jina la NMB MINING CLUB umezinduliwa tarehe 28 Juni, 2021 katika Hotel ya Morena Jijini Dodoma na  kuhuhudhriwa na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini.


Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Biteko amesema kuwa, ili kuwarahisishia wachimbaji kupata mikopo kwa urahisi katika mabenki ikiwemo vifaa vya uchimbaji, Wataalam wa Wizara ya Madini hawanabudi kutoa ushirikiano kwa mabenki pindi  yanapohitaji msaada wa kitaalamu ili yaweze kutoa mkopo kwa wateja wao kwani baadhi ya mabenki yameshindwa kutoa mkopo kwa wachimbaji kutokana na kukosa elimu ya kutosha kuhusu sekta ya madini.


" Ninatoa rai kwa mabenki nchini kuungana kwa pamoja na kutoa mikopo mikubwa kwa wawekezaji wakubwa wa madini  wanaotaka kuwekeza nchini ili faida inayotokana na mikopo hiyo ibaki nchini," amesema Waziri Biteko.


 Akijibu hoja mbalimbali zilizowasilishwa na watoa mada, Waziri Biteko amesema Wizara ya Madini inapokea mapendekezo yatakayowasilishwa katika kuangalia njia sahihi ya wachimbaji wa madini kukopesheka kupitia jukwaa hilo na kusisitiza njia  rahisi ni kupitia vyama vyao vya uchimbaji pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo pia  linafanya kazi ya kuwalea wachimbaji wadogo.


" Kwa kupitia STAMICO tumeanzisha mchakato wa kuangalia dhamana kwa wale wote wanaokwenda kukopa kwenye mabenki ili kujiridhisha na utaratibu huo utakamilika hivi karibuni," amesisitiza Biteko.


Aidha, Waziri Biteko ametoa wito kwa jukwaa hilo kuendelea  kutoa elimu kwa wadau wa Sekta ya Madini kuhusu umuhimu wa  kupendana na kuthaminiana kwani bila upendo Sekta ya Madini haiwezi kufika popote.


Waziri Biteko ameipongeza Benki ya NMB kwa ubunifu huo kwenye Sekta ya Madini na kueleza kuwa kupitia klabu hiyo iliyoanzishwa na benki ya NMB itapata fursa ya kupata wateja wengi waliopo kwenye Sekta ya Madini.



Naye, Afisa Mkuu wa Mikopo wa Benki ya NMB Daniel Mboto amesema lengo la kuandaa jukwaa hilo ni kutoa nafasi ya kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya wadau na benki ya NMB na kuongeza kwamba, uzinduzi huo mkoani Dodoma ni mwanzo wa kuzungumza na wadau wa Sekta ya Madini katika kutoa huduma mbalimbali ili kuwapa uelewa zaidi wa huduma za NMB.


 Jukwaa hilo la NMB Mining Club lililozinduliwa leo na Waziri Biteko mkoani Dodoma,  linatarajia kufanyika katika mikoa mingine saba hapa nchini .


Wengine waliohudhuria Uzinduzi huo  ni pamoja na Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA) John Bina,  Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Dodoma Chagwa Marwa, wataalam kutoka Wizara na Tume ya Madini, wafanyakazi wa Benki ya NMB  na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini.


CAPTION


  1. Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza wakati wa Uzinduzi wa NMB Mining Club uliofanyika tarehe 28 Juni, 2021 Jijini Dodoma 


  1. Waziri wa Madini Doto Biteko (Kushoto) na Afisa Mkuu wa Mikopo wa Benki ya NMB Daniel Mboto (Kulia) wakati wa Uzinduzi wa NMB Mining Club uliofanyika tarehe 28 Juni, 2021 Jijini Dodoma


  1. Picha ya pamoja ya Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati), Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula( Kulia) Afisa Mkuu wa Mikopo wa Benki ya NMB Daniel Mboto(Kushoto) na Watendaji kutoka Benki ya NMB wakati wa Uzinduzi wa NMB Mining Club uliofanyika tarehe 28 Juni, 2021 Jijini Dodoma


  1. Baadhi ya Washiriki waliohudhuria Uzinduzi wa NMB Mining Club uliofanyika tarehe 28 Juni, 2021 Jijini Dodoma




Share To:

Post A Comment: