Meneja wa TIC Kanda ya Kaskazini, Bw.Daudi Riganda akisisitiza jambo wakati wa uliolenga kuwaunganisha wawekezaji wakubwa na wajasiriamali wadogo na wakati (SMEs) uliofanyika kwenye ukumbi wa Veta Jijini Tanga


AFISA Kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga Buluba Kanuda akieleza jambo wakati wa mkutano huo kulia ni Meneja wa Maendelea ya Biashara wa Benki ya NBC Tanga Aljiran Mbwani
Meneja wa Maendelea ya Biashara wa Benki ya NBC Tanga Aljiran Mbwani akieleza jambo wakati wa mkutano huo kulia ni Afisa Biashara wa Jiji la Tanga

Sehemu ya Washiriki katika mkutano huo wakifuatilia kwa umakini
Sehemu ya Washiriki katika mkutano huo wakifuatilia kwa umakini

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeeleza kwamba kila nchi  hata zile zilizoendelea duniani zinahitaji wawekazaji ambao watawasaidia kuweza kukuza uchumi wao, pato la taifa, kuongeza mapato ya kikodi na yasiyo ya kikodi, kuzalisha ajira hasa kwa vijana, kuingiza teknolojia za kisasa, na kuongeza mitaji ya nje (FDI).

Hayo yalisemwa na Meneja wa Kituo cha Uwekezaji Kanda ya Kaskazini (TIC) Bw. Daudi Riganda wakati wa mkutano uliolenga kuwaunganisha wawekezaji wakubwa na wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) uliofanyika katika ukumbi wa VETA mjini Tanga.


“Kwetu sisi Tanzania wawekezaji ni muhimu sana na hata nchi ambazo zimeendelea nazo zinahitaji wawekezaji mfano  ukienda Dubai, Uingereza,  Brazil na kwingine kote wawekezaji wanahitajika kwa sababu wana mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na ndio maana  Rais wetu mpendwa mama Samia Suluhu Hassan moja wapo ya agenda zake ni uwekezaji”, alisema.

“Lakini nieleze kwamba kama uwekezaji hamna hata pato la Taifa litashuka hivyo tunahitaji uwekezaji kwa ajili ya kutusaidia kupata mapato ya kikodi na yasiyokuwa ya kikodi kwa sababu kupitia uwekezaji makampuni yatalipa kodi na matokeo mengine mengi zikiwemo ajira kuonekana “, alisema Meneja huyo.

Aliongeza kusema “ikiwa sekta binafsi itakuwa dhaifu basi matokeo kama ajira, kodi, teknolojia za kisasa nk pia yatapungua. Katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea duniani, sekta binafsi ndio injini ya maendeleo, na uwekezaji muhimu unatoka sekta binafsi".

Awali akizungumza katika mkutano huo, Meneja Utawala wa Kiwanda cha Maweni Limestone Aron Mushi alikishukuru Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa namna walivyowakutanisha na wajasiriamali na wadau wengine kuweza kuangalia changamoto ambazo wanakutana nazo ili kufanya uwekezaji uweze kukua, na wakati huo huo kusaidia ukuaji wa SMEs.

Alisema pia wanashukuru kwa kupata fursa ya kueleza yanayowakabili na kuweza kuishauri serikali kuona yale yanayofaa kwa ukuaji wa miradi yao na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Aidha, kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya Afri Line Tanga, Bi. Veronika John aliishukuru TIC kwa hatua ya kuwakutanisha wao kama wajasiriamali  na wawekezaji kuongea nao na kuweza kujua changamoto wanazokumbana nazo kwa namna moja au nyingine.

Alisema kwa sababu wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) wakati mwingine wamekuwa wakilalamika kuhusu wawekezaji kumbe wao ndio chanzo cha changamoto zinazowakabili na hivyo kushindwa kuwalipwa kwa wakati.

Hata hivyo alitoa wito kwa SMEs kujaribu kufanya kazi kwa kupenda shughuli au huduma wanazotoa ili kuweze kuwa endelevu kwa kuboresha ubora muda hadi muda.  


Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: