Nteghenjwa Hosseah, Manyara


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Ummy Mwalimu amesema Wauguzi ni miongoni mwa wataalamu wa Afya wanaopaswa kuheshimiwa na kupewa thamani inayostahili na wasichukuliwe kisiasa.


Waziri Ummy ameyasema hayo wakati alipokuwa akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya Wauguzi Duniani yakiyofanyika Mkoani Manyara tarehe 12 Mei,2021.


Amesema  uuguzi ni fani adhimu na kuwataka viongozi wa Mikoa na Wilaya kuacha kuwadhalilisha kwa kuwaweka ndani kwa tuhuma zisizo na ushahidi. 


“Viongozi wa Mikoa na Wilaya niwatake kuelewa kuwa uuguzi ni taalamu adhimu na muache kuamuru wawekwe ndani au kuwachukulia hatua kali ambazo haziendani na taalum yao kwa tuhuma ambazo hazina ushahidi, hili tuliache mara moja,”amesema


Ameongeza "Kama Muuguzi amekosea akashitakiwe kwenye Baraza la Wauguzi na Wakunga ambapo atachukuliwa hatua kwa matakwa ya taaluma yake na sio kwa utashi wa kisiasa.” 


Hata hivyo, amesema kiongozi yeyote atakayemuweka ndani muuguzi  awe amethibitisha ameiba lakini  kwa tuhuma nyingine akashitakiwe kwenye Baraza lao la Kitaaluma.


Pia Mhe.Ummy amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuacha kuwakatalia wauguzi kwenda kusoma mara wanapopata fursa za kwenda kujiendeleza kielimu.


"Wauguzi lazima wathaminiwe kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhudumia wagonjwa sababu mara zote ukienda hospitali Daktari atakuona kwa muda mchache sana na wakati mwingi utakuwa na nesi katika kukuhudumia hivyo wapewe moyo,"amesema.


Amewapongeza na kuwashukuru Wauguzi kwa kazi kubwa walioifanya wakati wa wimbi la ugonjwa wa Corona na amewataka kuendelea kutimiza wajibu wao na kuokoa maisha ya watu.


Akijibu hoja zilizowasilishwa na Wauguzi katika risala yao, Waziri Ummy amesema suala la muundo linafanyiwa  kazi na lilishawasilishwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa hatua zaidi.


 Mhe. Ummy amesema kwa sasa  Madaktari na wauguzi wafanye  kazi kama timu moja ili kuleta matokeo chanya kwa jamii inayowategemea na hayo ya kiutawala yataendelea kuangaliwa na kufanyiwa kazi.


Kuhusu posho ya majukumu,  amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI itaangalia ni namna gani inaweka mazingira bora kwa wauguzi walioko TAMISEMI kwa kadri rasilimali zitakavyopatikana.


"Ofisi yangu itahakikisha inatoa kipaumbele katika kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba za watumishi wa Afya kwa kujenga nyumba za kutosha ili watumishi hao waweze kukaa kwenye vituo vyao na kufanya kazi kwa amani,"amesema.


Katika hatua nyingine, Mhe. Ummy ametoa zawadi ya sh.500,000 kwa Muuguzi Aldolefina Shayo

wa Zahanati ya Kilangare iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Same ambaye amevunja rekodi ya kuhudumia wagonjwa hamsini kwa siku bila kunung’unika na leo ameshindwa kushiriki maadhimisho hayo kwa kuwa yuko peke yake kwenye zahanati hiyo na hakuna mtu wa kumsaidia.


Waziri Ummy amesema katika ajira mpya zilizotangazwa watapelekwa wauguzi wawili na Mganga mmoja ili kuboresha zaidi huduma za Zahanati hiyo.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: