Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo Omari (kushoto), akiwa naa liyewahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF na Kocha wa Timu ya Taifa Stars, Ami Ninje (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Dkt. Richard Masika wakikagua eneo la chuo kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa chuo hicho ili kujenga Kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo.

Timu ya wataalam mbalimbali wa michezo na ardhi ikipitia ramani ya maeneo ya ujenzi wa madarasa na hosteli.

Timu ya wataalam ikiangalia eneo la ujenzi wa madarasa wa Kituo cha kuendeleza vipaji vya Michezo

 



Na John Mapepele, Dodoma

 

Serikali inatekeleza mradi wa  kupanua eneo la  Chuo cha  Maendeleo ya Michezo Malya ikiwa ni  mkakati  maalum wa kuanzisha Kituo cha Kuendeleza Vipaji vya Michezo  ili kuibua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo hapa nchini.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo Omary ameyasema haya  wakati alipokuwa na  Timu ya wataalam walipotembelea na kukagua eneo  hilo hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya kufanya maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kitakuwa na hadhi ya kimataifa.

 

“Niseme tu kwamba  kukamilika kwa kituo  hiki kutaifanya  nchi yetu kusonga mbele kwenye  Sekta ya Michezo kwa kuwa  vipaji vya wanamichezo wetu vitaibuliwa na  tutaweza sasa  kushindana  na mataifa mengine duniani sasa” amefafanua Mkurugenzi Omary

 

Amesema Tanzania ina hazina kubwa ya vipaji kilichokuwa kinakosekana ni kituo maalum cha michezo cha kuwanoa wachezaji na kwamba kukamilika kwa kituo hiki ni suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.

 

Awali, Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema  Wizara imeendelea  kufanya mageuzi makubwa ili kutimiza ahadi  za Serikali na matarajio ya wananchi kwa ujumla.

 

Amesema Wizara  inatekeleza kwa kwa kasi  masuala yote  yaliyobainishwa kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka  2020-2025 ikiwemo ibara125(a)-(h) kwa Sekta ya Habari, ibara239 (a)-(m) kwa Sekta ya Utamaduni, ibara 249 (a)-(j) Sekta ya Sanaa na ibara 243(a)-(k) kwa Sekta ya Michezo.

 

Akihutubia kwenye kikao cha Wafanyakazi wa wa Wizara hiyo hivi karibuni, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema tayari Wizara yake imeshakamilisha agizo la Serikali la kuanzisha Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ikiwa pia ni mkakati wa kukuza sekta ya Michezo nchini.

 

“Wizara imekamilisha agizo hili kwa kuhuisha Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni ambao umetengewa shilingi bilioni 1.5. 

Mfuko  huu kwa  mwaka ujao wa fedha utajikita katika ujenzi wa miuondombinu muhimu ikiwemo jengo la SANAA HOUSE hapa Dodoma, pia utaendelea  kutengewa fedha zaidi kwa lengo la kutekeleza  majukumu mawili adhimu; kuwajengea uwezo wanatasnia hizo za Sanaa na Utamaduni kupitia mafunzo na  kuwawezesha kupata mikopo na ruzuku katika kazi zao” amesisitiza Waziri Bashungwa


Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: