Na Grace Semfuko, MAELEZO.

Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amewaonya watu na vyombo vya habari vinavyokiuka taratibu za utoaji wa taarifa kwa jamii kuhusiana na mambo mbalimbali ya Serikali na kusema kuwa, zipo mamlaka zilizothibitishwa na kwa ajili ya utoaji wa taarifa hizo.

Dkt. Abbasi amesema katika siku za hivi karibuni kumekuwa na tabia mpya ya baadhi ya vyombo vya habari, Watu na Mitandao ya kijamii, ambao wanatoa taarifa mbalimbali zinazohusu Serikali na Taasisi zake bila kuzingatia misingi ya utoaji wa taarifa hizo suala ambalo linakwenda kinyume na matakwa ya Sheriai na kuwataka kuacha hufanya hivyo.

“Sasa naona kama kuna tabia mpya imejitokeza ya baadhi ya watu, mtu anajitokeza anaanza kutoa takwimu zake kuhusu maradhi mbalimbali, kuhusu vifo, kuhusu wagonjwa, hili kwa niaba ya serikali naomba kusisitiza sio sahihi, na tuviombe vyombo vya Habari viachane kabisa na watu wa namna hiyo, kila mwanajamii asasi za kijamii mbalimbali, viongozi wa dini, wa siasa, kila mwanajamii anapaswa kushiriki katika kutoa elimu kuhusu hatua za kuepukana na kuhamasisha kuitoa jamii hofu na kusisitiza masuala yale ambayo yapo kwenye miongozo lakini masuala ya takwimu na kisera yanapaswa kubaki kwa serikali” amesema.

Amesema Serikali imekuwa ikitoa taarifa zake kwa kuzingatia taratibu na kwamba yoyote anaehitaji taarifa zozote za Serikali milango ipo wazi kabisa na kwamba wawasiliane mamlaka husika ili wapate taarifa sahihi za takwimu wanazotaka kuzitoa.

“Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na tabia mpya ya baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii au maeneo mengine ya nchi kujitolea tu taarifa, zingine zikiwa zinahusu Serikali, zingine zikiwa zinahusu taasisi mbalimbali za Umma bila kuzingatia misingi ya utoaji wa Taarifa hizo, ni juzi tu Mheshimiwa Rais aliagiza viongozi mbalimbali watoe taarifa kwa umma waeleze miradi na matukio mbalimbali yanatokea katika taasisi zao, nimeona leo nisisitize tena kwamba, Serikali ina utaratibu wake wa kutoa taarifa” alisema.

Amesisitiza kuwa watu ambao hawahusiki katika agizo hili la utoaji wa taarifa zinazohusu maslahi ya umma kama magonjwa mbalimbali yakiwepo ya milipuko na mengineyo, hiyo ni kazi ya Serikali na sio ya mtu binafsi.

“Kwa hiyo watu wengine ambao hawahusiki na taratibu hizo hawapaswi kuingilia huo mfumo na hiyo itifaki  kama ilivyo kwenye maeneo mbalimbali, mfano kwenye maeneo ya magonjwa ya kuambukiza, magonjwa ya mlipuko, zipo taratibu za sheria ya huduma na sheria ya Afya ya jamii zimeeleza wazi kabisa kwamba ni kiongozi wa nafasi gani anaweza kutoa taarifa, lakini vilevile mfano mwaka jana Tanzania ilipopata agonjwa wa Corona, Mheshimiwa Rais alitoa itifaki ya viongozi watakaosemea ugonjwa huu, sasa mtu anapoibuka na kusema anakosea” amesisitiza.

Aidha aliwataka watu kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Share To:

Post A Comment: