Wizara ya Kilimo katika kuhakikisha inawezesha wakulima wengi nchini kupatiwa miche bora ya kahawa imepanga kuingia makubaliano na Jeshi la Kujenga Taifa ili kutumia ardhi yake kuzalisha mbegu za mazao ili kutosheleza mahitaji ya wakulima..
Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki
alipofanya ziara ya kukagua shamba la kahawa lenye ukubwa wa ekari
hamsini katika kambi ya 822 JKT Kiteule cha Tarime wilayani Tarime.
“Wizara
ya Kilimo ipo tayari kuingia makubaliano na JKT kuzalisha miche bora
mingi ya kahawa ili kutosheleza mahitaji ya wakulima wa mkoa wa Mara na
jirani kwa kuanzia nitatoa shilingi milioni 19 ili TACRI waanzishe
kitalu cha miche hapa kambini” alisema Kusaya.
Aliongeza
kusema jitihada za Jeshi la Kujenga Taifa Kiteule cha Tarime
zinatekeleza kwa vitendo agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli la kuona
majeshi yetu yanajitegemea kimapato kwa kuanzisha miradi ikiwemo kilimo
cha kahawa.
Akiwa
kambini hapo Tarime, Kusaya alikagua shamba la kahawa ekari 52
zilizopandwa kati ya lengo la ekari 200 na kupongeza jitihada hizo na
kuwataka Taasisi ya Utafiti wa zao la kahawa (TACRI) kuanza maandalizi
ya kufungua kitalu cha miche bora ya kahawa shambani hapo ili
wajitosheleze kwa miche na kugawa mingine kwa wakulima.
“Tutahakikisha
tunawasaidia JKT ili wakimaliza kupanda ekari zote 200 kahawa taasisi
zetu za TFRA na zingine zitawezesha upatikanaji mbolea na pembejeo
ikiwemo mfumo wa umwagiliaji ili shamba hili litumike kama darasa la
wakulima wa Tarime kuja kujifunza kilimo bora cha kahawa” alisisitiza
Kusaya.
Katika hatua nyingine Kusaya aliagiza Jeshi la Kujenga
Taifa kutumia fursa iliyopatikana nchini Misri kuzalisha mahindi ya
njano ambayo yanahitajika kwa kiwango cha tani 25,000 kwa mwezi ifikiapo
Julai mwaka 2021 kwani wana uwezo huo na wataalam wapo.
Kwa
upande wake Kaimu Kamanda Kikosi cha 822 KJ Kiteule cha Tarime Meja MM
Kinana alimweleza Katibu Mkuu huyo wa Kilimo kuwa tayari katika msimu
huu 2020/21 wamefanikiwa kupanda ekari 52 za kahawa na mahindi kati ya
lengo la ekari 200.
Aliongeza
kusema kiteule cha Tarime kina eneo linalofaa kilimo cha kahawa ekari
430 ambapo mkakati wa Jeshi ni kulima eneo hilo kila mwaka kuongeza
ekari 50 na kuwa changamoto iliyopo ni ukosefu wa mfumo wa maji ili
kumwagilia kahawa wakati wa kiangazi.
“Kiteule
chetu tayari tumepanda miche 52,000 ya kahawa na kuwa lengo letu ni
kuzalisha wenyewe miche bora ili tujitosheleze kupanda ekari zote 200 na
kugawa ziada kwa wakulima wa jirani hivyo tunaomba wizaraya kilimo
ituunge mkono” alisema Meja Kinana.
Alitaja
changamoto ya upatikanaji mbolea ya kupandia aina ya DAP hivyo kutatiza
jitihada za kilimo kwani inayopatikana inauzwa gharama kubwa licha ya
serikali kutoa bei elekezi lakini Tarime haifiki alisisitiza Meja
Kinana.
Akijibu
changamoto hizo za JKT, Katibu Mkuu Kusaya alisema kwanza
watashirikiana na wizara ya Maji ili kuona namna ya kuweka miundombinu
ya maji kwenye shamba hilo kwa kutumia chanzo kilichopo na hatimaye Tume
ya Taifa ya Umwagiliaji itafika kuona namna ya kuwa na mfumo wa
umwagiliji kwa njia ya matone ili kahawa ikue vema.
Pili,
ameelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) kwenda Tarime kukutana
na uongozi wa wilaya na kikosi cha 822 KJ kujua mahitaji ya mbolea na
kuwasaidia kuagiza kwa mfumo ya pamoja (Bulk Procurement Sytem-BPS) ili
wapate kwa gharama nafuu na kwa wingi.
Tatu,
ameitaka TACRI kuharakisha kufungua kitalu cha miche 250,000 ya kahawa
kiteuleni hapo na kuwa ifikapo mwezi Januari 2021 atakwenda tena Tarime
kukagua utekelezaji wa maagizo yake.
“Sifa
ya jeshi ndio sifa ya nchi hivyo wizara yangu itafanya kila lililo
ndani ya uwezo kuzitumia taasisi zake kushirikiana na JKT kukuza sekta
ya kilimo na kwamba nitakwenda makao makuu ya JKT kukutana na Mkuu wa
Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Charles Mbuge kujadili mkataba huu
wa mashirikiano ikiwemo wa kuzalisha mbegu za mazao mengine ”
alisisitiza Kusaya.
Akiwa
shambani hapo Kusaya alizungumza na vijana wa kujitolea wanaofanya kazi
za shamba na kuwapongeza kwa kuwa wazalendo kulitumikia taifa
Kusaya
alisema “nawasihi vijana mkirejea nyumbani baada ya mkataba wenu
kuisha nendeni mkawe wazalendo kwa kuanzisha shughuli za kilimo na
ujasiliamali kwani miaka mitatu mliyokaa JKT imewafanya muwe wataalam wa
kilimo “
Aliwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutoa ajira kwa vijana na kipaumbele ni kwa vijana ambao tayari wameonesha uzalendo na moyo wa kujituma wakiongozwa na waliopo kwenye makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa.
Mwisho
Imeandaliwa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
TARIME
22.11.2020
Post A Comment: