JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu wawili akiwemo Muuguzi wa Hospitali ya Serikali ya Rufaa mkoani Shinyanga wakituhumiwa kwa makosa ya wizi wa vifaa tiba vya hospitali hiyo ya mkoa vyenye thamani ya sh. milioni 26.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga ACP, Debora Magiligimba amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Madaraka Joseph (32) mkazi wa Mageuzi kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni muuguzi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga.

Mtuhumiwa mwingine aliyekamatwa ametajwa kuwa ni Suka Charles (42) mkazi wa Mtaa wa Buzuka Manispaa ya Shinyanga ambapo pia anamiliki zahanati ya iliyopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Akifafanua zaidi Kamanda Magiligimba amesema mnamo Oktoba 13, mwaka huu saa 12.00 jioni kulitokea wizi wa mashine mbili za kuangalia wagonjwa katika chumba cha upasuaji aina ya EDAN 1MB na DATA SCOP 1 zenye thamani ya shilingi milioni 26.

Kamanda Magiligimba amesema baada ya kutokea kwa wizi huo, Jeshi la Polisi lilianza kufanya uchunguzi ambapo lilibaini kuwa mtuhumiwa Madaraka Joseph ambaye ni mtumishi kwenye chumba cha upasuaji katika Hospitali ya mkoa ndiye aliyeiba vifaa tiba hivyo.

“Tulibaini baada ya kuiba vifaa hivyo alikwenda kuviuza kwa Suka Charles kwa makubaliano ya shilingi 4,000,000 na alitanguliziwa kiasi cha shilingi 2,000,000 hata hivyo tulimkamata Suka baada ya kumfanyia upekuzi nyumbani kwake maeneo ya Mhongolo wilayani Kahama na kufanikiwa kukamata vifaa hivyo,” alieleza Magiligimba.

Amesema pia Polisi walikamata vifaa vingine vinavyotumiwa na vifaa hivyo ikiwemo, Patient monitor S/N 301237 – M16 CO9160006-01, Patient monitor S/N PG 63700-B2, BP Machine Accessories (5), Cable wires Accessories (7), Medical molecular sieve, Oxygen Concentrator (1) Serial no. 598 na Oxygen Concentrator Intesty S/N 601-1.

Kamanda Magiligimba amesema watuhumiwa wote wawili wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika ambapo ametoa wito kwa watumishi wa umma kuacha tabia ya wizi wa mali za umma zinazosababishwa na tamaa ya mafanikio ya muda mfupi.


Share To:

msumbanews

Post A Comment: