Monday, 30 November 2020

MRISHO GAMBO KUWAPATIA BIMA ZA AFYA WALEMAVU WOTE JIJI LA ARUSHA Na Geofrey Stephen Arusha


MBUNGE wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amesema atahakikisha watu wote  wenye ulemavu 565  katika Jiji la Arusha  atawapatia viti mwendo 100 na kuwapatia matibabu kwa kupindi cha miaka mitano kupitia Mfuko wa  Bima ya Afya (NHIF).


Aidha amesema atachimba visima vya maji kwenye soko kuu la Arusha,Samunge,Kijenge na kwa kuanza ameshachimba kisima katika soko la Kilombero.Akizungumza ofisini kwake  jijini Arusha  na  Waandishi wa Habari,Gambo alisema mbali na masoko hayo pia atachimba visima kwenye shule zenye uhitaji wa maji ili wanafunzi wapate huduma hiyo bila kuhangaika."Lakini katika uongozi wangu nitaweka nguvu kubwa katika kutatua kero za wafanyakazi wa viwandani na kwa kuanza nitafanya ziara ya siku nne kwenye kiwanda cha A to Z,Sunflug,Lothia na Tanfoam na nitaongozana na wataamu toka Idara ya kazi, Osha,NSSF,PSSF,Mfuko wa Fidia kwa wafanyaka pamoja na viongozi wa vyama vya wafanyakazi,"alisema Gambo.


Alisema ziara hiyo imetokana na kupokea malalamiko mengi ya wafanyakazi hao wakati alipotembelea kwenye viwanda hivyo kuomba kura wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na kuahidi kuzifanyia kazi mara baada ya kuchaguliwa.

Aidha alisema waajiri wengi hawatoi mikataba kwa wafanyakazi wao,lakini viongozi wa serikali wanapowatembelea huonyeshwa mikataba hewa,huku wafanyakazi wakiendelea kuteseka.

Kuhusu ukusanyaji wa taka katika jiji hilo alisema amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wnaanchi za kutozwa gharama kubwa za uzoaji wa taka na kwamba atajenga hoja kwenye barasa la madiwani ili gharama zipunguzwe.

Kwa upande wa sekta binafsi amepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wawekezaji kunyimwa vibali vya kuajiri raia wa kigeni kwa madai kwamba kuna watanzania wenye uwezo wa kufanya kazi hizo.


"Hoja ya kunyimwa wawekezaji kuajiri raia wa kigeni siyo kweli kama itanyima watanzania kupata ajira na katika hili nitapeleka hoja bungeni itakayounda sheria ya kuajiri raia wa kigeni watano na wengine wawe watanzania,"alisisitiza.

Aidha kwa upande wa mikopo Gambo alisema amefanya uchunguzi na kubaini vikundi vya watu wenye ulemavu,vijana na wanawake kila kundi linapewa mikopo na matokeo yake kila mtu anakwenda kufanya biashara yake na ikitokea mmoja wao ameshindwa kurejesha kikundi kizima kinachukuliwa hatua kitu ambacho siyo sahihi.


"Hili nalo nitalijengea hoja bungeni ili kuwe na utaratibu wa kukopesha mtu mmoja mmoja na sio kikundi ili kila mtu abebe mzigo wake mwenyewe pale atakaposhindwa kirejesha,"alisema.

No comments:

Post a Comment