Mwenyekiti wa madereva na wamiliki wa Bajaji na bodaboda Manispaa ya Singida Ahmed Juma akitoa ufafanuzi wa tamko la kulaani vijana wanaotaka kufanya vurugu
Dereva wa Bodaboda Manispaa ya Singida Ramadhani Zuberi akitoka ufafanuzi kwa waandishi ambao hawapo pichani kupinga na kulaani maandamano ya vijana ambao wanataka kutumika kuvuruga amani
Sehemu ya madereva wa bodaboda Manispaa ya Singida

John Mapepele na Rose Nyangasa, Singida

Wamiliki na Madereva wote wa Bajaji Mkoa wa Singida wametoa tamko rasmi la kulaani baadhi ya vijana ambao wameanza kutumiwa na baadhi ya vyama vya upinzani kuandamana kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, Mwaka huu.

Akitoa  tamko  kwa  niaba ya  wanachama 2000 wa  Mkoa wa Singida  kwenye Kituo cha Bajaji  Soko Kuu la Mjini Singida, Mwenyekiti wa Madereva na Wamiliki wa Bajaji na Boda boda  Manispaa ya Singida, Ahmed Juma amesema  umoja wao  umepinga njama  zinazofanywa  na  baadhi ya  vyama  ya kuwatumia madereva  hao na kusisitiza kuwa njama hizo hazitafanikiwa katika Mkoa  wa Singida .

“Tumejipanga kukabiliana na uhuni wowote ambao umepangwa kufanywa kwenye kipindi  hiki na baadhi ya wahuni wachache wasioitakia mema  nchi yetu, tunaomba  vyombo  vya ulinzi visimamie hili kikamilifu na sisi tupo nyuma yao” aliongeza Juma

Amesema kinachotaka kufanyika sasa baada ya  uchaguzi kukamilika na matokeo  kutangazwa  kwa kufuata taratibu zote za uchaguzi na Mamlaka halali ni  vurugu na uvunjifu wa amani jambo ambalo amesema halikubaliki badala  yake amewasihi wananchi wafanye kazi  ili  kuiletea nchi yetu maendeleo  zaidi katika awamu ya sasa.

Amemwomba Rais, John Pombe Joseph Magufuli  kuendelea kuiletea maendeleo Tanzania ili itoke kwenye Uchumi wa Kati  hadi Uchumi wa juu kabisa  na hatimaye  kuboresha maisha  ya watanzania wote.

Mwenyekiti wa Madereva wa Boda boda  wa  eneo  la Soko Kuu Mjini Singida, Kulwa Moshi  ameonya madereva wa  Bodaboda ambao kwa namna moja au nyingine  watatumika katika kuvunja Sheria za nchi kwa kupanga  njama za kufanya maandamano  yasiyo ya amani.

Moshi ameongeza kuwa wananchi wameamua kuwachagua viongozi wanao wapenda hivyo hakuna sababu ya watu kuandaa njama za kupinga matokeo ya uchaguzi.

Naye Ramadhani  Zuberi,  Dereva wa  Bajaji kwenye  Kituo Kikuu cha Mabasi  ya Mkoa wa Singida amepongeza Serikali kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu kwa uwazi  ambao umeweza kufuata taratibu zote na kutoa matokoa kwa wakati

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Nchini (NEC), Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli anatarajiwa kuapishwa Novemba 5 Mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: