Na. Majid Abdulkarim , Dodoma


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Victor Kategere amesema kuwa Mifumo ya tehama imekuwa chachu ya udhibiti wa upotevu wa mapato katika kukuza uchumi wa Taifa.


Kategere amebainisha hayo leo  Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha ziara ya viongozi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibari kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamuhanga .


Aidha Kategere amesema uwepo wa mifumo madhubuti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa imepelekea kuongezeka kwa mapato yanayosaidia kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.


Akiwasilisha taarifa ya Mifumo Mkurugenzi wa TEHAMA OR- TAMISEMI, Erick Kitali amesema uwepo wa mifumo umesaidia Serikali kupunguza gharama kubwa kwa watendaji wa halmashauri waliokuwa wakisafiri  kuja Dodoma kutengeneza bajeti na mipango ya halmashauri zao kwani sasa zinatengenetwa kupitia mifumo na kuwasilisha wizarani.


 “Ili ukusanye mapato kwa haki lazima kutoa huduma bora kwa wananchi hivyo hakuna kinachoshindikana kwenye TEHAMA kwani leo tunaona  watanzania walivyo rahisishiwa upatikanaji wa Huduma kupitia mifumo iliyotengenezwa na wazawa kwa kutoanza kupanga foleni katika maofisi ya umma ” ameeleza Kitali.


Pia Kitali ameeleza kuwa mifumo hiyo imetengenezwa na watanzania hivyo ni rahisi kutatua changamoto pale zinapojitokeza katika mifumo hiyo na wapo wataalamu kwa ajili  ya usalama wa mifumo hiyo ili kutoingiliwa na kutumiwa vibaya.


Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa TAMISEMI, Shomari  Mukhandi  ameeleza ukusanya wa mapato ya ndani ya Halmashauri yanakusanywa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa Sura Na. 287,288 na 290.


Vile vile Mukhandi amesema Halmashauri zimepewa mamlaka ya kukusanya kodi , ushuru, ada na tozo mbalimbali ili kutekeleza majukumu yake ya kisheria yakiwemo kutoa huduma za kijamii ,  kuimarisha ulinzi na kudumisha amani kwa kuinua uchumi wa wakazi wa himaya za mamlaka hizo.


“Nitoe rai  kwa Viongozi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ) kuhakikisha mnakusanya mapato kna kutenda haki katika ukusanyaji wa mapato bila kuwakandamiza  wananchi”, amesisitiza Mukhandi.


Naye Mkurugenzi wa Sera na Mipango OR-TAMISEMI , John Cheyo, amesema TAMISEMI inafanya vema katika shughuli zake na hayo ni matokeo ya ugatuzi wa madaraka , uwajibikaji na ushirikiano mzuri uliopo  katika watendaji wa ofisi hiyo.

 

Share To:

msumbanews

Post A Comment: