Wednesday, 7 October 2020

PROF. MWAKALILA AELEZEA MAFANIKIO YA CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE NDANI YA MIAKA MITANO YA JPM

 


MKUU wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila amesema katika kipindi cha miaka mitano ya serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli chuo hicho kimefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi kwa kampasi zote kutoka wanafunzi 1592 wa mwaka 2014/2015 hadi wanafunzi 9,799 mwaka 2019/2020.

Prof. Mwakalila amesema hayo leo wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari chuoni hapo.

Amesema mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi Cha miaka mitano chini ya uongozi wa awamu ya Tano  ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wahitimu ambapo katika kampasi ya Kivukoni idadi ya wahitimu imeongezeka kutoka wahitimu 569 katika mwaka wa masomo 2014/2015 hadi kufikia wahitiumu 3,237 katika mwaka wa masomo 2018/2019.

“Chuo kimeongeza idadi ya watumishi kutoka watumishi 168 mwaka 2015 hadi watumishi 285 ambapo kati yao kampasi ya Kivukoni Dar es Salaam wapo 231 na kampasi ya karume Zanzibar wapo 5”, alisema Prof. Mwakalila na kuongeza kuwa chuo kimeongeza idadi ya walimu wahadhili wenye shahada ya uzamivu (PhD) kutoka 2 wenye PhD mwaka 2015 hadi wahadhili 35 mwaka huu wa 2020.

Prof. Mwakalila  amesema kuwa  chuo hicho pia kimeongeza idadi ya kozi za mafunzo ya kitaaluma kutoka kozi 3 za shahada zilizokuwepo mwaka 2015 hadi kufikia jumla ya kozi 10 za shahada na kozi moja ya shahada ya umahiri mwaka 2020.

Alisema kwa sasa chuo kina kozi 10 ngazi ya shahada,kozi 11 ngazi ya stashahada na kozi 11 ngazi ya Astashahada.

Alisema chuo kimeboresha mitaala yote ikiwa ni pamoja na kuingiza somo la uongozi, maadili na uzalendo ili kila mwanafunzi awe na ufahamu wa kutosha kuhusu uongozi maadili na uzalendo.

Pia chuo kimefanikiwa kuongeza idadi ya vitabu zaidi ya 20,000 katika makataba za chuo kwa kampasi zote,chuo kimekamilisha ujenzi wa ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 300 kwa pamoja na ofisi 10 za wafanyakazi ujenzi ulianza mwaka 2017 na kukamilika mwaka 2019.

Mkuu huyo wa Chuo aliongeza kusema kuwa chuo kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na uwekaji wa viti visivyohamishika kwenye kumbi zote, ufungaji wa vifaa vya kisasa projekta katika kumbi za mihadhara ununuzi wa kompyuta kwa ajili ya maabara za kompyuta.

Prof. Mwakalila alibainisha kuwa  chuo kimefanikiwa kusomesha wahadhiri zaidi ya 40 katika mafunzo ya shahada ya uzamivu katika fani mbalimbali za kitaaluma aidha watumishi katika idara mbalimbali za kitaaluma na uendeshaji wamejengewa uwezo kupitia mafunzo ya muda mfupi.

Prof.Mwakalila alisema chuo pia kimeweza kufanikiwa kupata eneo Mkoani Dodoma lengo likiwa ni kusogeza huduma ya vhuo kutoa elimu na mafunzo kwa wahitaji na kwamba mpaka sasa wako kwenyer hatua nzuri itakapokamilika ujenzi utaanza.


IMETOLEWA NA:

KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO

CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE

7/10/2020

No comments:

Post a comment