Wednesday, 14 October 2020

HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAPANDIKIZA FIGO KWA WAGONJWA 13
Na Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

 

Hospitali ya Benjamini Mkapa Jijini Dodoma imefanikiwa kufanya upandikizaji wa  figo kwa wagonjwa 13 Nchini kwa kipindi cha miaka mitano na kuendelea kuwa kinara  katika utoaji wa huduma bora za afya.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dodoma Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt.  Alphonce Chandika amesema tangu kuanzishwa kwaHospitali hiyo mwaka 2015 imekuwa na mafanikio ambayo yamechangiwa na serikali kuimarisha uwekezaji  katika vifaa tiba vya kutolea  huduma kwa wananchi.

 

“Mwaka 2018 kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo watu kutoka nchini Japan tulianza huduma ya upandikizaji wa figo hivyo tangu kuanza kwa hospitali hiyo tumeshapandikiza figo wagonjwa 13 na hayo ni mafanikio makubwa kuna hospitali zina zaidi ya miaka 50 hazijawahi kufanya hivyo kwa hiyo tusiwategegemee sana watu wa nje “amesema

 

Dk Chandika ameongeza kuwa wakati hospitali hiyo inazinduliwa ilikuwa na changamoto ya kuazima  wahudumu wa afya wa 22 lakini hadi sasa imefanikiwa kuwa na watumishi 456.

 

 

Wakizungumzia mafanikio ya hospitali hiyo kwa kipindi cha miaka mitano Mkurungezi kitengo cha upasuaji Dk Hinju Januarius pamoja na Muuguzi Mkunga Debora Mobwasa wamebainisha kuwa wamefanya kazi kwa juhudi kubwa ili kuwasaidia wananchi licha ya kuanza utoaji wa huduma kwa changamoto mbalimbali mwaka 2015.

“Kwa kweli tunashukuru kwa hospitali ya Benjamin Mkapa kwa juhudi kubwa hizi nasi kama wataalm wa Afya tumekuwa bega kwa bega kufanya juhudi kubwa na kwa ufanisi katika hospitali hii”

 

 

Nao baadhi ya wanachi jijini Dodoma wameipongeza hospitali hiyo kwa kutoa huduma sitahiki kwa jamii kwa kipindi cha miaka 5.

 

 

Hospitali hii ya Benjamin Mkapa, ilianzishwa mwaka 2015 kwa tamko la Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dkt.  Jakaya Mrisho Kikwete na ilizinduliwa rasmi Oktoba 13  ya Mwaka huo.

No comments:

Post a comment