Na. Catherine Sungura,WAMJW-Tabora

Imeelezwa kuwa kuboreshwa kwa miundombinu imesaidia kwa kiasi kikubwa huduma ya damu salama kwenye Kanda ya Magharibi ambayo inahudumia mikoa ya Tabora,Katavi,Singida na Kigoma.

Kaimu Meneja wa kanda hiyo Bi. Zaitun Abdalah ameyasema hayo wakati wa kampeni ya kukusanya damu kwenye shule ya sekondari Mabama iliyoko Manispaa ya Tabora.

“Kwa kiasi kikubwa uboreshwaji wa barabara umesaidia sana kurahisisha upatikanaji wa mahitaji wa damu salama kwenye mikoa hii tunayoihudumia ambayo inayo eneo kubwa kijiografia hivyo inapohitajika damu kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma tunawapatia kwa wakati”Alisema.

Kwa upande wa wiki hii ya kampeni ya kukusanya damu iliyoanza tarehe 21 mwezi huu na kumalizika tarehe 25 ,Kaimu Meneja huyo amesema Kanda yake imeweza kukusanya chupa 186 kwa siku mbili ikiwa imekaribia lengo lililoweka la kukusanya chupa 100 kwa siku na chupa 500 zinazotarajiwa kukusanywa kwa wiki.

Aliongeza kuwa kwa mkoa wa tabora timu yake imejipanga katika ukusanyaji wa damu katika wilaya ya Igunga na timu nyingine katika manispaa pamoja na halmashauri ya wilaya ya Uyui na wamelenga kuwafikia wanafunzi wa sekondari kwani upatikanaji wa kundi hilo ni rahisi katika kipindi hiki.

“kama kanda hatujachoka kuhamasisha wananchi licha ya changamoto ya uelewa kwa jamii kuhusu uchangiaji damu,hivyo tumejipanga kuendelea kutoa elimu kwenye makundi yote ili tuweze kuwa na damu za kutosha kwenye hospitali zetu”.

Hata hivyo alisema kama Kauli mbiu ya kampeni hii  inavyosema “changia damu,ili kuokoa maisha ya akina mama wanaoleta uhai duniani “hivyo jamii inapaswa kuelewa uchangiaji wa damu mara kwa mara ni muhimu ili kuokoa vifo vya akina mama wajawazito  wanapoteza uhai wakati wanapotimiza haki yao ya kuleta watoto duniani.

Naye Afisa Mhamasishaji wa kanda hiyo Constantine Chiba alisema wamejiwekea utaratibu kutoa elimu ya kuchangia damu kwa kutembelea vijiji mbalimbali kwenye mkoa huu,nyumba za ibada pamoja na makundio mengine katika jamii ili kuweza kuwa na akiba ya damu na pindi inapohitajika waweze kuokoa maisha ikiwemo ya akina mama wanaojifungua.

Chiba alisema yapo makundi matano ya wahitaji wa damu yakiwemo akina mama akina mama wajawazito na watoto wachanga,wahanga wa ajali,wanaohitaji tiba ya upasuaji,wenye matatizo ya kuishiwa damu (sikoseli) na kundi la mwisho ni watu wote ambao wanaweza kuugua na kuhitajika kuongezewa damu“kumbe sisi sote ni wahitaji wa damu kwani hatuyawezi kuyakwepa makundi haya yote kama binadamu kwani ugonjwa au ajali haiwezi kukwepa jinsia au umri wa mtu”.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: