Na John Walter-Manyara


Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange,   amiepongeza Benki ya CRDB kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo nchini ili kuharakisha maendeleo ya Watanzania. 

Twange  ametoa pongezi hizo katika hafla ya uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta,Power Tiller,Planters,Harrow na Spea mbalimbali za vifaa vya kilimo iliyofanyika katika Benki ya CRDB tawi la Babati mkoani Manyara.

Amesema kupitia mkopo huo wa Trekta utaongeza mnyororo wa thamani  ambapo mwenye Trekta atatoa ajira, ataingia sheli kununua mafuta,atanunua matairi, ataenda kwa fundi gereji.

Amesema ubunifu uliofanywa na CRDB unarahisisha uboreshaji wa maisha ya Watanzania kiuchumi na hasa katika kuunga mkono juhudi za serikali kuondoa umaskini wa kipato kwa wananchi wake.

Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, Chiku Issa alisema benki hiyo inaunga mkono juhudi za serikali za awamu ya tano inayothamini Maendeleo ya wakulima ambapo mpaka sasa wametoa shilingi Bilioni 707.2 kwa ajili ya Kilimo na kuchangia asilimia 40 ya mikopo yote inayotolewa nchini.

Amesema kwa kushirikiana na makampuni ya ETC Agro wauzaji wa matrekta ya Mahindra, Agricom wauzaji wa matrekta ya Swaraj na Kubota na Loan Agro wauzaji wa matrekta ta John Deer wapo tayari kuwahudumia wananchi wa Manyara.

Chiku ameeleza kuwa benki ya CRDB imeamua kuleta wadau wa maendeleo ya kilimo ili kuwapunguzia wakulima riba kubwa na kupata mikopo ya dhana za kilimo bila dhamana ambapo pia matrekta yatakuwa yanafanyiwa matengenezo na wauzaji hao wa matrekta.

Kwa upande wake mkulima alienufaika na mkopo huo,  Zuhura Maige, aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mkombozi wa wakulima wadogo kama yeye, huku akiwahamasisha wakulima wengine kujitokeza kuchangamkia fursa hizo za uwezeshaji wakulima zinazotolewa na Benki ya CRDB kupitia mikopo ya vifaa vya kilimo bila dhamana kuanzia mwaka mmoja hadi miaka mitatu.
Share To:

Post A Comment: