Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akitoa maelekezo mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Mary Makondo (wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dkt John Pima (Wa kwanza kushoto) pamoja na Msajili Msaidizi wa Hati katika ofisi ya Ardhi mkoa wa Arusha Juliana Ngonyani wakati akikagua masijala ya ardhi alipokwenda kuzindua ofisi hiyo jana.
 Baadhi ya Watendaji wa sekta ya ardhi mkoa wa Arusha na wananchi wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (hayupo pichani) alipokwenda kuzindua ofisi ya ardhi mkoa wa Arusha jana.
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikata utepe kuzindua ofisi ya ardhi mkoa wa Arusha jana. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Arusha Idd Kimanta, wa tatu kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo na Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Arusha Leo Komba.
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi pamoja na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa mkoa wa Arusha waliopatiwa hati za ardhi wakati wa uzinduzi wa ofisi ya ardhi ya mkoa wa Arusha jana.
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza wakati wa uzinduzi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Arusha jana. Wengine katika picha ni Mkuu wa mkoa wa Arusha Idd Kimanta (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo (Kulia) na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha Zelothe Stephen (Kushoto). (PICHA ZOTE NA HASSAN MABUYE WIZARA YA ARDHI)
Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka Maafisa Ardhi nchini kuhakikisha wanawafuatilia wamiliki wa ardhi ambao hati zao zimekamilika lakini hawataki kuzichukua ili wazichukue katika kipindi cha siku tisini.

Lukuvi alisema hayo jana jijini Arusha wakati akizindua ofisi ya ardhi ya mkoa huo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kuzindua ofisi za ardhi katika mikoa mbalimbali nchini.

Waziri Lukuvi ambaye tayari amezindua ofisi za ardhi kwenye mikoa ya Tanga na Manyara alisema, hivi karibuni Bunge lilipitisha sheria inayotaka mmiliki wa ardhi aliyepimiwa eneo lake kuchukua hati katika kipindi cha siku tisini na asipofanya hivyo utaratibu wa kumkata kodi ya pango la ardhi utafanyika.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, kumekuwa na tabia ya baadhi ya wamiliki wa ardhi kutojitokeza kuchukua hati za viwanja vyao kwa lengo la kukwepa kulipa kodi ya pango la ardhi jambo alilolielezea kuwa linamnyima fursa mbalimbali mmiliki sambamba na kuikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi ya ardhi.

Alitolea mfano wa mkoa wa Arusha kuwa, pamoja na mkoa huo kuwa na jumla ya viwanja 78,405 vilivyopimwa na hati zake kusajiliwa lakini ni hati 29,000 pekee ndizo zilizochukuliwa na wamiliki wake na hivyo kufanya hati 49,405 kutochukuliwa na kuikosesha serikali mapato ya ardhi.

‘’Ardhi ndiyo ulinzi wa rasilimali na inachangia kodi ya serikali kwa hiyo wale wote wasiochukua hati wajitokeze katika kipindi cha siku tisini, tunataka idadi ya viwanja vilivyopimwa na kuwekewa mawe ifanane na hati zilizopo na wote waliopimiwa wakachukue baada ya hapo kama hujachukua hati utaletewa invoice ya malipo’’ alisema Lukuvi.

Akizungumzia uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa, Lukuvi ambaye alitoa hati 201 kwa wamiliki wa ardhi mkoa wa Arusha alisema, ofisi hizo zimeanzishwa ili kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kubainisha kuwa, sasa wananchi watapata huduma zote za ardhi kwenye mikoa yao kama walivyokuwa wakipata Makao makuu ya Wizara na Ofsi za ardhi za Kanda.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Arusha Iddy Kimanti ameipongeza wizara ya ardhi pamoja na mhe Rais John Pombe Magufuli kwa uamuzi wa kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa na kubainisha kuwa ofisi yake itatoa ushirikiano na kusaidia masuala mbalimbali ya ofisi ya ardhi kwenye mkoa wake ili kufanikisha azma ya serikali.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kuwezesha utekelezaji jukumu la kusogeza huduma za sekta ya ardhi karibu na wananchi kwa uanzishaji ofisi za ardhi za mikoa.


Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Arusha Leo Komba alisema, tangu kuanzishwa ofisi yake mwezi Machi mwaka huu tayari jumla ya hati 210 zimeandaliwa na 101 kutolewa kwa wamiki wake huku miamala 282 ikiwa imefanyika na michoro 19 yenye viwanja 4,196 kuandaliwa sambamba na Ramani 29 zenye viwanja 133 kuidhinishwa.
Share To:

Post A Comment: