Na Joachim Nyambo,Mbarali.
WAKAZI wilayani Mbarali mkoani Mbeya wametakiwa kutobweteka na badala yake watambue kuwa bado wanapaswa kuendelea kuchukua tahadhali na kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Corona kwa kufuata taratibu zote zilinazotolewa na Viongozi Wakuu wa Nchi pamoja na Wizara ya Afya.
Tahadhari zaidi imetakiwa kuimarishwa majumbani hasa wazai wanaporejea wakitokea kwenye mizunguko ya utafutaji ambapo hukutana na watoto wakiwamo wadogo wasiotambua umuhimu wa kuchukua tahadhari na mara nyingi hulazimisha kukutana kwa haraka na wazazi wao kwa kuwalaki hata kabla hawajafuata kanuni za kujikinga ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali,Reuben Mfune, kwa sasa wilayani hapa kuna baadhi ya maeneo watu wanaonekana kuanza kujisahau na wameacha kuendelea kuchukua tahadhari.
Mfune aliyasema hayo alipokuwa akifungua warsha iliyoandaliwa na Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani Mbeya(Mbengonet) iliyolenga Kujenga uwezo kwa jamii na kuimarisha mifumo ya Serikali ili kupunguza kasi ya ongezeko la maambukizi ya COVID-19 na kuleta Mabadiliko chanya dhidi ya mila, desturi na tabia zinazochangia maambukizi katika mkoa wa Mbeya.
Mkuu huyo wa wilaya alisema bado ni mapema sana kuamini kuwa maambukizi ya Corona hayapo kabisa na jamii kurudi katika maisha yaliyokuwa yamezoeleka bali lazima tahadhali zinendelee kuchukuliwa kwa kufuata miongozi iliyowekwa.
Sambamba na tahadhali kwa wananchi,alisema bado jitihada za wadau zinahitajika katika kuisaidia Serikali kuendelea kutoa elimu ya kujikinga na Corona na kuupongeza mtandao huo kwa kuwa sehemu ya wadau waliamua kujitoa katika utoaji elimu ndani ya jamii.
Mfune aliutaka mtandao wa Mbengonet kufika maeneo yote yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama miji midogo iliyopo barabara kuu ya TANZAM lakini akasihi watakapokuwa wanatoa elimu hiyo wasiwajengee hofu wananchi, ila wawape ujumbe na kuwaelekeza kuendelea kujikinga na kuchukua tahadhari sambamba na kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuinua vipato vyao na uchumi wa nchi.
“Watu wengi wanatafsiri vibaya kauli ya Rais Dkt John Pombe Magufuli.Rais Magufuli hajasema Corona imeisha Tanzania, ila kasema Corona imepungua kwa kiasi kikubwa nchini kwetu. Kuna baadhi ya watu kwenye jamii wanapuuza taratibu za afya zilizowekwa ili kupunguza uwezekeano wa kuenea kwa ugonjwa huu hasa katika sehemu zenye mikusanyiko.”

“Siku hizi tunajikinga na Corona tunapotoka nyumbani kwenda kwenye mihangaiko yetu, ila tunasahau kuzikinga familia zetu pale tunaporudi nyumbani, ni vyema kila mtu akachukua tahadhari kwa kuweka ndoo yenye maji tiririka na sabuni nyumbani kwake.” Alisema Mfune

"Utakuta pale nyumbani watoto wadogo na hivi kwa sasa hawaendi shuleni wameshinda hawakuoni baba au mama sasa unaporudi wao hawajui kama kuna Corona wanataka moja kwa moja ukae nao uwanyenyue kwakuwa ndiyo furaha kwao.Hapo tunapaswa kuwa makini kunawa kwanza."aliongeza

Awali Katibu Mtendaji wa Mtandao wa Mbengonet, Paul Kita alisema kuwa Shirika limejipanga kwenda kutoa elimu ya kujikinga na COVID- 19 na kuhamasisha matumizi ya Barakoa na vitakasa mikono kwa waendesha Bodaboda, Madereva wa Bajaji, kwenye minada pamoja na kwenye Mikusanyiko kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Serikalini.

Kita aliongeza kuwa baadhi ya watu katika jamii wameanza kukusanyika kwenye baadhi ya maeneo bila kuchukua tahadhari na wamegundua baadhi ya maeneo mengi ni machafu kitu ambacho kitasababisha magonjwa mengine ya mlipuko kwani kinachoua watu kwa sasa sio Corona pekee hata uchafu na magonjwa mengine

Mbengonet ni mtandao ambao umekuwa na mchango mkubwa mkoani Mbeya katika Uelemishaji, Uhamasishaji na Ushawishi wa shughuli za maendeleo katika sekta za Afya, Kilimo, Maji, Elimu, Utawala bora pamoja na Haki za binadamu.
Share To:

Post A Comment: