Na Esther Macha, Mbeya

Wakati ligi mbalimbali zikiwa zimekaribia kuanza kurindima  katika viwanja tofauti tofauti nchini,Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya umekabidhiwa ndoo ishirini na vitakasa mikono kutoka Taasisi ya Tulia Trust kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa COVID 19.

Makabidhiano hayo yalifanyika ndani ya Uwanja wa Sokoine ambapo Taasisi ya Tulia Trust iliwakilishwa na Meneja wake Jacqueline Boaz.

Akipokea vifaa hivyo Meneja wa Uwanja wa Sokoine Modestus Mwaluka kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya ambao ni wamiliki alisema vifaa hivyo vitatumika kama ilivyokusudiwa.

Aidha Kaimu Katibu wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya Mwalimu Lucas Kubaja alisema vifaa vilivyotolewa vimekuja kwa wakati ili kutekeleza agizo la serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID 19.

Moshi Seleman ni Mwenyekiti wa timu ya Isanga Rangers aliipongeza Taasisi ya Tulia Trust kwa kutoa vifaa hivyo.

Katibu wa Chama Cha Waamuzi Sadiki Jumbe mbali ya kuipongeza Taasisi ya Tulia Trust kutoa vifaa hivyo aliomba wadau kujitokeza kusaidia vifaa vingine kuelekea michezo mbalimbali katika uwanja huo.

Naye Ramadhan Lulandala ambaye ni mjumbe wa chama cha mpira wa miguu Wilaya ya Mbeya (MUFA)alisema Taasisi ya Tulia Trust imefungua milango kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia vitakasa mikono.

Hivi sasa viwanja vingi nchini vimeendelea na maandalizi ya kuandaa viwanja kutekeleza agizo la serikali la kuvitaka viwanja vyote kuwa na maji tiririka na vitakasa mikono kabla ya mashabiki na wachezaji kuingia viwanjani.

Tangu kuingia ugonjwa wa COVID 19 Taasisi ya Tulia Trust imetoa ndoo na vitakasa mikono Kata zote za jiji la Mbeya,vituo vya mabasi na ofisi zote za Chama cha Mapinduzi.
Share To:

Post A Comment: