Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Mawasiliano), Dkt. Zainab Chaula amezikumbusha taasisi za Serikali
kutumia huduma za Shirika la Posta Tanzania (TPC) kusafirisha bidhaa,
vifurushi na vipeto kwa usalama zaidi.
Dkt.
Chaula ameyasema hayo wakati wa kikao cha Menejimenti ya Wizara yake na
viongozi wa TPC wakiongozwa na Posta Masta Mkuu wa TPC, Hassan
Mwang’ombe kilichofanyika jana kwenye ukumbi wa Wizara hiyo uliopo
Mtumba, Mji wa Serikali, Dodoma ambapo Shirika hilo lilifika ofisini
hapo kwa lengo la kujitambulisha na kuwasilisha taarifa ya Shirika hilo
kwa Dkt. Zainab Chaula, Katibu Mkuu mpya wa Wizara hiyo.
Dkt.
Chaula alisema kuwa TPC imepewa dhamana kisheria kuwa msafirishaji mkuu
wa barua, vifurushi, vipeto na bidhaa mbali mbali kwa mujibu wa sheria
ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Na. 19 ya mwaka 1993
iliyoanzisha Shirika hilo nani Shirika la umma ambapo Serikali
imewekeza.
Ameongeza
kuwa TPC imefanya kazi kubwa ya kusafirisha sampuli kutoka hospitali
mbali mbali nchini kwenda Maabara Kuu ya Serikali wakati wa kipindi cha
janga la virusi vya Corona pamoja na kusafirisha nyaraka za mahakama
zote nchi nzima, benki, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,
Mifuko ya Hifadhi za Jamii, hisa za kampuni mbali mbali na kutumia
usafiri wa ndege kwenda ndani na nje ya Tanzania.
Ameitaka
TPC kuunganisha huduma za posta na anwani za makazi na postikodi na
simu za mkononi ili kuhudumia wananchi katika kufanikisha azma ya
Serikali ya kurahisisha na kufanikisha usambazaji na usafirishaji wa
barua, vifurushi, vipeto na bidhaa kwa wananchi.
“Tunataka
mwananchi afikishiwe nyanya nyumbani kwake na sio atumie piki piki
kuzunguka kwa muda mrefu na kupiga simu bila kufika kwa mteja kwa
wakati,” amesisitiza Dkt. Chaula.
Naye
Posta Masta Mkuu wa TPC, Hassan Mwang’ombe ameziomba taasisi za
Serikali kutumia Shirika hilo kusafirisha barua, vifurushi na vipeto kwa
kuwa bidhaa zao zitafika kwa usalama na uhakika kwa kuwa Shirika hilo
linatumia huduma ya mtandao wa TEHAMA kutoa huduma zake kwa wateja kwa
kuunganisha ofisi zake 202 zilizopo maeneo mbali mbali nchi nzima; wana
wataalamu wa lojistiksi; na wanatumia anwani za makazi na postikodi
kuhudumia wateja.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amelishauri Shirika hilo
kuwa pamoja na kuboresha huduma zake ndani ya nchi pia amelitaka
kufungua milango yake na kufanya biashara na nchi nane za jirani
zinazopakana na Tanzania kwa kuongeza huduma za lojistiksi kwenda nchi
za jirani za usafirishaji wa bidhaa, biashara mtandao, uwakala na maduka
ya kubadilisha fedha ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti mara kwa mara
ili kuendeleza biashara za Shirika hilo.
Naye
Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara wa Shirika hilo, Mwanaisha Ally Said,
ameiomba Wizara kuhakikisha kuwa watoa huduma za usafirishaji wa
nyaraka, vifurushi na vipeto wasio na leseni ya kuendesha biashara hiyo
inayotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wanachukuliwa
hatua kwa mujibu wa sheria ili kuhakiisha kuwa wananchi wanapata huduma
za sekta ndogo ya posta na Serikali inapata mapato yake
Post A Comment: