Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
RAIS Dkt. John Magufuli ametoa siku 30 kwa Viongozi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kumsimamia usiku na mchana mkandarasi wa kampuni ya Padiel JV kuhakikisha anakamilisha kwa haraka  kazi ya ujenzi wa barabara ya Kilosa- Dumila yenye urefu wa Kilometa 24.

Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo jana (Jumatatu Juni 29, 2020), Rais Magufuli alisema hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo inayofanywa kasi ya mkandarasi huyo kutokana ujenzi wa barabara hiyo kuchukua muda mrefu kukamilika.

Alisema kumekuwepo na malalamiko ya makampuni mengi ya kizalendo yakilalamika kutopewa kazi za miradi ya serikali, lakini pindi yanapopewa kazi hiyo yameshindwa kutekeleza ujenzi wa miradi hiyo, hatua inayosababisha  kuchelewesha maendeleo ya wananchi.

Aidha Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD) kuhakikisha kuwa iwapo kuna vikwazo vinavyokwamiza utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo ikiwemo malipo yanashughulikiwa kwa haraka.

‘’Sifurahishwi na kazi ya mkandarasi ningekuwa mimi ni Kamwelwe (Waziri) basi leo asingekuwepo huyu mkandarasi, haiwezekani tuwape kazi halafu ifanyike ya hovyo hivi, natoa rai kwa makandasi wote wanaotekeleza miradi ya ndani wabadilike’’ alisema Rais Magufuli.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha uongozi wake, Serikali ya Awamu ya Tano kamwe haitowatetea wakandarasi wazembe na kuitaka kampuni ya Padiel JV kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo inakamilika haraka kwa kuwa kwa kipindi kirefu wananchi wa Wilaya ya Kilosa wamekuwa wakiishi katika mateso makubwa ya barabara hiyo.

Aidha Rais Magufuli aliiagiza Wakala wa Barabara Nchini Mkoa wa Morogoro kuanza kufanya usanifu na upembuzi yakinifu wa kipande cha barabara iliyosalia ya Kilosa-Mikumi yenye urefu wa Kilometa 70 ili kipande hicho kiweze kukamilika kwa haraka.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TANROAD, Mhandisi Patrick Mfugale alisema ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha Wilaya ya Handeni (Tanga)-Turiani-Dumira-Kilosa-Mikumi, una gharama ya kiasi cha Tsh. Bilioni 32 na kukamilika kwake kunatarajia kupunguza changamoto ya wasafiri kusafiri umbali mrefu pasipo na barabara ta mchepuko.

Alisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulianza februari 2019 na unatarajia kukamilika mwezi Januari 2020 ambapo ujenzi huo unatarajia kuwanufaisha makandarasi wazalendo kupata ujuzi katika ujenzi wa barabara.
Share To:

Post A Comment: