Na WAMJW – Dar es Salaam
Waandishi wa Habari nchi wametakiwa kuandika habari sahihi kuhusu virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-19) ili wananchi wapate taarifa ambazo zitawasaidia  kujikinga na ugonjwa huo.

Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akipokea msaada wa vifaa kinga,vifaa vya kupima joto la mwili, vipeperushi,  mabango na vifaa vya  kutoa elimu kwa Umma kwa ajili ya waandishi wa Habari vilivyotolewa na Shirika la UNESCO.

Waziri Ummy alisema wizara yake imekuwa ikishirikiana na  vyombo vya habari  kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kwa wakati  kuhusu ugonjwa wa Corona na kufahamu hatua za kufuata ili wajikinge na ugonjwa huo.

“Msaada huu unagusa wadau muhimu sana kwani hawa ndiyo wanaotusaidia kupeleka taarifa kwa wananchi. Mmenifurahisha zaidi kuzifikia  redio za jamii 34 ambazo zitapata vifaa vya kupima joto la mwili pamoja na vifaa kinga vingine. Redio hizi ni za muhimu sana kwani zinawafikia wananchi wengi waliopo vijijini”,.

 “Kwa upande wa waandishi wa habari , pamoja na majukumu yenu ya kazi za kila siku mnazozifanya hakikisheni mnatoa taarifa sahihi za Corona na siyo habari za kuwatisha wananchi bali waelimisheni. Nanyi hakikisheni mnafuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kujikinga na ugonjwa huu hii ikiwa ni pamoja na kusimama umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mtu wakati mnapotekeleza majukumu yenu”, alisema Waziri Ummy.

Akikabidhi vifaa hivyo mwakilishi mkazi wa Shirika la UNESCO Tanzania Tirso Dos Santos aliipongeza Serikali kwa hatua zinazochukuwa katika kupambana na ugonjwa wa Corona.

“Vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za ugonjwa huu kwa wananchi, nasi tumeona tuwape vifaa kinga, mabango na  vipeperushi ambavyo zitawasaidia kuufahamu zaidi ugonjwa wa Corona na kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi kwa wakati”, alisema Santos.

Vifaa vilivyotolewa na Shirika la UNESCO ambavyo vitatolewa kwa waandishi wa habari ni  vitakasa mikono, barakoa, mashine za kupima joto la mwili, mabango na  vipeperushi.

Mwisho
Share To:

msumbanews

Post A Comment: